Madiwani Geita Mji Wapatiwa Elimu ya Vishikwambi
Madiwani wote wa Halmashauri ya Mji Geita wamepata mafunzo ya matumizi ya vishikwambi (Tablets) kwa ajili ya shughuli mbalimbali katika kata zao ikiwa ni pamoja na kutumika katika vikao mbalimbali vya kisheria vinavyofanyika.
Akitoa mafunzo hayo hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri Magogo, Kaimu Mkuu wa kitengo cha TEHAMA Halmashauri ya Mji Geita Bi. Hamida Abdulkhrarim amewasisitiza waheshimiwa Madiwani kuwa vikao vyote vya kisheria vitafanyika kwa kutumia teknolojia ya kidijitali kupitia vishikwambi hivyo na kuwashauri kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili wapate uzoefu wa kuvitumia.
Afisa TEHAMA wa Geita Mji ameongeza kuwa Waheshimiwa Madiwani wanapaswa kutumia wenyewe vishikwambi na kuacha mazoea ya kuwapatia watu wengine ili kuepusha uharibifu utakaojitokeza ikiwepo kuvunjika, kupotea na kuweka taarifa za vikao katika mazingira salama.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Yefred Myenzi amewashukuru Serikali mtandao na kusema kuwa mfumo unaotumika katika vishikwambi hivyo ni salama kabisa na utasaidia kutunza taarifa kwa muda mrefu tofauti na kutumia makablasha kama awali ambapo makaratasi yalikuwa rahisi kuchanika na kupotea, hivyo Madiwani wanatakiwa kujifunza kwa moyo mkunjufu ili kuelewa vyema zaidi matumizi ya vifaa hivyo.
“Vishikwambi vitasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa taasisi ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji wa vikao kwa kutumia vifaa vya TEHAMA vinavyotumia nyaraka laini badala ya nyaraka ngumu kama karatasi.” Aliongeza Mkurugenzi Myenzi.
Kwa upande wao Waheshimiwa Madiwani wamefurahi kupata elimu hiyo ambapo wataendelea kujifunza zaidi ili wawe wabobezi na kuahidi kutunza kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali ili viweze kutumika kwa lengo lililokusudiwa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa