Madiwani Geita Mji Wafanya Ziara Ya Mafunzo Chalinze
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Geita wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Costantine Morandi, baadhi ya wataalam, wawakilishi wa wakulima pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe wametembelea Halmashauri za Wilaya ya Chalinze, Mvomero na Halmashauri ya jiji la Tanga kwa lengo la kujifunza mbinu bora na mikakati ya kuboresha ukusanyaji mapato.
Wakiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani hivi karibuni ujumbe wa Madiwani kutoka Halmashauri ya Mji Geita wametembelea mradi wa kuzalisha kokoto ambao unamilikiwa na Halmahauri hiyo, ambapo walijifunza namna Halmashauri ya Chalinze ilivyofanikiwa kudhibiti upotevu wa mapato kwa kufunga kamera kwenye vizuizi(Barriers) na desturi ya kuwabadilisha vituo vya kazi wakusanyaji mapato mara kwa mara.
Katika ziara yao waliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, Waheshimiwa Madiwani walipata fursa ya kutembelea mradi wa Machinjio ya mifugo na Ushirika wa wakulima wadogo wadogo kilimo cha umwagiliaji mpunga Dakawa(UWAWAKUDA LTD) ambapo walitembelea shamba lao na kujifunza namna kilimo cha umwagiliaji kilivyoweza kuwainua kiuchumi wanaumoja hao.
Mwenyekiti wa Bodi ya UWAWAKUDA Ndg. Joseph Lutango ameeleza kuwa ushirika wao wenye wanachama 941 ambao una eneo lenye jumla ya hekta 3,225.15 kati ya hizo 2000 zikiwa na miundombinu ya umwagiliaji na zinatumika katika uzalishaji wa mpunga.
Ndg. Joseph Lutango ameeleza kuwa ushirika wao unawapatia faida mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa mikopo mikubwa ya zana za kilimo kama vile matrekta na mashine ya kuvunia mpunga(combine harvester), kuchangia katika huduma za jamii kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu katika kata ya Dakawa, upatikanaji wa ajira kwa vijana 5000 kutoka katika kata ya Dakawa na maeneo Jirani Pamoja na wanachama kupata uwezo wa kujikimu kimaisha wao binafsi Pamoja na familia zao.
Ujumbe wa waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Geita wakiwa ziarani katika Halmashauri ya jiji la Tanga walitembelea mradi wa kiwanda cha kuzalisha matofali ambayo yanatengenezwa kwa mchanganyiko wa mchanga, saruji na kokoto nyembamba. Matofali ambayo yanatumika katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali na watu binafsi. Mradi wa matofali umeiwezesha Halmashauri ya jiji la Tanga kuingiza mapato ya Shilingi milioni 176 kwa mwezi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Pamoja na timu yake wametoa shukrani za dhati kwa viongozi wa maeneo yote ambayo walipata fursa ya kuyatembelea kwa kuwapokea kwa upendo na ukarimu na kuwajengea uzoefu wa miradi mbalimbali ambayo inawaingizia mapato kwa kiasi kikubwa na kuahidi kuyafanyia kazi mazuri yote ambayo wamejifunza katika ziara hiyo ili kupanua wigo wa ukusanyaji mapato ya Halmashauri ya Mji wa Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa