Madarasa Mapya Kumaliza Uhaba Kalangalala Sekondari
Ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa unaoendelea katika shule ya sekondari Kalangalala Geita mjini utaondosha tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo pindi ujenzi wa madarasa hayo utakapokamilika mwishoni mwa mwezi Juni 2024.
Kauli hiyo imebainishwa na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Godfrey Mahewa alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa madarasa hayo kwa wajumbe wa kamati ya Fedha na Uongozi waliokuwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mwalimu Mahewa amesema kuwa shule yake ilipokea shilingi 239,400,000 (Milioni 239.4) kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kujenga vyumba tisa vya madarasa pamoja na matundu nane ya vyoo.
Mwalimu Mahewa ameongeza kuwa madarasa yanayojengwa shuleni hapo yatawezesha shule ya Sekondari Kalangalala kuwa na vyumba 42 vya madarasa, hivyo kuondokana na uhaba wa madarasa uliokuwa unawakabili hapo awali na kuwezesha wanafunzi 1873 wa shule hiyo kusoma kwa nafasi kutokana na utoshelevu wa vyumba vya madarasa.
Mradi huo ambao umefikia asilimia 60% ya ujenzi wake utaondoa tatizo la uhaba wa viti na meza kwa wanafunzi kwa sababu unaenda sambamba na ununuzi wa viti na meza 450. Pia kupunguza tatizo la mrundikano wa wanafuzi darasani , kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kuzuia tatizo la utoro kwani madarasa yatawavutia wanafunzi wapende kufika shule kuhudhuria masomo.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Prudence Temba ametoa pongezi kwa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuongeza madarasa katika shule ya Sekondari Kalangalala, hiyo ni ishara ya upendo alionao mama kwa vijana wake. Kadhalika amewapongeza wananchi wa Mtaa wa Moringe Kata ya Buhalahala wakiongozwa na Diwani wao kwa moyo wa kujitolea nguvu kazi ili kukamilisha mradi huo, pamoja na uongozi wa shule kwa usimamizi mzuri wa mradi huo wenye kiwango cha hali ya juu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa