Mabaraza Ya Ardhi Yakumbushwa Kuwa na Weledi
Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Ndugu Thomas Dimme amewakumbusha wataalam wanaoshughulikia Mabaraza ya ardhi katika Wilaya ya Geita kufanya kazi kwa haki na weledi mkubwa wanapowahudumia wananchi wenye migogoro mbalimbali.
Ndugu Dimme ametoa ujumbe huo wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya utoaji huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Geita iliyofanyika katika ukumbi wa Gedeco Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita ameeleza kuwa kundi kubwa linaloathirika na vikwazzo vya upatikanaji wa haki pamoja na msaada wa kisheria ikiwemo migogoro ya ardhi na mipaka ni wanawake na watoto kutokana na kushindwa kukidhi gharama zinazohitajika wakati wa huduma na kutofikiwanna huduma hizo kiurahisi.
Ndg. Dimme ametumia fursa hiyo kuzipongeza taasisi zinazoshirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa kutambua umuhimu wa msaada wa kisheria kwa jamii na kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi wenye kipato kidogo katika kutambua na kutatua masuala yanayowasibu pindi migogoro inapotokea.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Geita Samuel Maweda ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Mji Geita kwa kuandaa Maadhimisho hayo na kuomba liwe zoezi endelevu kwa kila mwaka ili wananchi wapate fursa ya kutatuliwa migogoro ya kisheria inayowakabili kama mirathi, migogoro ya ardhi na mengineyo.
Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa huduma ya kisheria hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwajengea wananchi wote uelewa juu ya sheria na msaada wa kisheria pamoja na kanuni zake ambapo kauli mbiu ya mwaka 2020 inasema “Usimamizi Bora wa Mirathi Kwa Maendeleo ya Familia”.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa