Kitalu nyumba cha Mfano chajengwa Geita Mji
Idara ya Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mkandarasi wamefanikiwa kujenga kitalu nyumba( green house) ya mfano ambayo itatumika kuwafundisha vijana walio chini ya umri wa miaka 35 juu ya umuhimu na faida ya kulima mazao ya mbogamboga katika kitalu nyumba.
Akizungumzia faida za kilimo cha kitalu nyumba wakati wa mazungumzo baina yake na mwandishi wa habari hii katika eneo ambapo kitalu nyumba kinajengwa, Afisa kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bw. Samwel Ng’wandu amesema kuwa kilimo cha kitalu nyumba husaidia mazao kujikinga dhidi ya wadudu na magonjwa kutoka nje pia mkulima hupata faida kubwa kupitia kilimo cha muda mfupi katika eneo dogo.
Bw. Samwel Ng’wandu ameongeza kuwa kilimo cha kitalu nyumba hutunza unyevu kwenye ardhi kwa muda uliokusudiwa katika kukuza mimea. Kadhalika kilimo hicho hutumia madawa kidogo kwa ajili ya kukinga mimea dhidi ya magonjwa tofauti na matumizi makubwa ya madwa kwa kilimo cha eneo la wazi (open field).
Kwa upande wake Mratibu wa kitalu nyumba katika Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Lenaida Baitani amesema kuwa matarajio ya Idara yake ni kuwa baada ya mafunzo kukamilika vijana watakaolengwa wataweza kutengeneza vitalu nyumba vyao kwa kutumia vifaa vya ujenzi vitakavyokuwa na gharama watakazozimudu. Pia mafundi waliotengeneza kitalu nyumba cha mfano watapata ajira ya kutengeneza vitalu nyumba vingine katika maeneo yao.
Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya ujenzi wa vitalu nyumba vya mfano katika Mkoa wa Geita Ndg. Boniface Mwanje ameeleza kuwa kitalu nyumba kilichojengwa katika makao makuu ya Halmashauri ya Mji kimegharimu zaidi ya shilingi milioni 12 za kitanzania. Kitalu nyumba hicho kina upana wa inchi 8 na urefu inchi 30 ambacho kinataraji kukamilika mapema mwezi machi mwaka 2019 na kitadumu kwa zaidi ya miaka kumi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa