Kamati Ya Siasa Wilaya Yaridhishwa na Miradi Geita Mji
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Geita wameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa usimamizi bora wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati, vyumba vya madarasa na utoaji mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2022 hadi Disemba 2023.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Barnabas Mapande ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi wake na kutoa fedha ambazo zimetumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyumba vipya 71 vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 na ujenzi wa Bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum.
‘’ Napenda kutumia fursa hii kuwasihi watendaji wote wa Serikali kuhakikisha mnasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazoletwa na Serikali kwa kujenga majengo yenye ubora uliotarajiwa. Kadhalika nawaomba ndugu zangu wa wilaya ya Geita kuendelea kujitolea nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo Serikali yetu tukufu inatoa fedha kwa lengo la kuboresha Maisha ya kila mtanzania.” Aliongeza Ndg. Mapande.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Geita Bi. Naomi Fujo ameipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mkopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambao wanafanya shughuli mbalimbali za kujikwamua kiuchumi. Bi. Naomi amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kufanya kazi kwa bidi na uaminifu ili waweze kufanya marejesho kwa wakati.
Miradi iliyotembelewa na Kamati ya Siasa Wilaya ni pamoja na ujenzi wa madarasa mapya tisa katika Shule ya Sekondari Mkolani, bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum Shule ya Msingi Kasamwa, Zahanati ya Nyakahengele, upanuzi wa chanzo cha maji Nyankanga na kutembelea vikundi viwili vilivyonufaika na mikopo isiyo na riba kutoka Halmashauri ya Mji Geita ambavyo ni kikundi cha vijana Maisha Kata ya Nyankumbu ambacho kinajishughulisha na utengenezaji wa mikanda ya Gypsum na Kikundi cha wanawake Tema kinachopatikana katika Kata ya Kalangalala na kinajishughulisha na utengenezaji wa mvinyo wa asili kwa kutumia ndizi mbivu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa