Kamati Ya Siasa Mkoa Yamwagiza Mkandarasi Kukabidhi Barabara
Kamati ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita imemtaka Mkandarasi Civmark Company Limited wa Dar es Salaam aliyepewa zabuni ya kutengeneza barabara ya Upendo dispensary –American chips yenye urefu wa km 0.35 inayojengwa kwa kiwango cha lami kukabidhi barabara hiyo ifikapo tarehe 30 Juni 2021.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni wakati wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Mheshimiwa Alhaj Said Kalidushi walipotembelea kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya mji Geita.
Mhe. Alhaj Kalidushi amefafanua kuwa kazi inayofanywa na mkandarasi huyo imekuwa ikisuasua sana ambapo barabara imetengenezwa kwa kipindi cha takribani miezi sita, hali inayopelekea wananchi wa eneo jirani na barabara hiyo hususan wafanyabiashara wa maduka ya nguo na bidhaa nyinginezo kupata adha ya vumbi kali kutoka kwenye barabara hiyo.
Kamati ya Siasa Mkoa pia imetoa pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa ujenzi wa bweni la kisasa la wasichana katika shule ya Sekondari Bulela ambalo limejengwa kwa shilingi milioni 120 kutoka katika vyanzo ambavyo ni mfuko wa jimbo, CSR kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Geita Bi. Rahel Ndegeleke ameushauri uongozi wa shule ya Bulela kuhakikisha mwezi Julai wanafunzi watakapofungua shule wasichana 80 waanze kutumia hosteli hiyo ili wanafunzi wanaotokea katika vijiji vya Gamashi ,Igwata, Bumanji na Nyambogo wanapata adha ya kutembea umbali mrefu kufika shuleni waondokane na kero hiyo.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati hiyo walipomtembelea nyumbani kwake katika mtaa wa Mbugani kata ya Kalangalala Bi. Janeth Francis ambaye ni mjane anayenufaika na mradi wa kunusuru kaya maskini chini ya mfuko wa TASAF ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumwezesha fedha ambayo ameitumia kuwanunulia mahitaji ya shule watoto wake watatu, kukarabati nyumba anayoishi na kuchimba kisima kifupi cha maji.
Miradi mingine iliyotembelewa na kamati hiyo ni pamoja na utendaji kazi wa soko kuu la wajasiriamali Katundu na ujenzi wa miundombinu ya maji na umeme katika kijiji cha Shinamwendwa kata ya Nyanguku
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa