Kamati Ya Siasa Mkoa Wakoshwa Na Miradi Geita Mji
Wajumbe wa Kamati ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita wametoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambao unaridhisha.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila walifanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM katika miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Mji Geita.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita ametoa pongezi kwa kikundi cha vijana Upendo wanaojishughulisha na uchomeleaji vyuma ambao wamekopeshwa mkopo usio na riba kutoka serikalini ambao umewawezesha kuimarisha biashara yao inayowaingizia kipato na kuwakwamua kiuchumi.
“Hongereni sana kwa uaminifu na uadilifu mlioonyesha na kutumia fedha mlizokopeshwa na halmashauri katika malengo mliyojipangia tofauti na wanavikundi wengine ambao wakishapatiwa mikopo hiyo wanagawana na kila mmoja anakwenda kuzalisha fedha hizo kwa shughuli zake binafsi.” Aliongeza Ndg. Nicholaus Kasendamila.
Wajumbe wa Kamati ya siasa Mkoa wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watanzania na kutoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawanufaisha wananchi katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, kilimo na mifugo, maji, nishati nk.
Miradi mingine iliyotembelewa na kamati ya siasa mkoa ni pamoja na upanuzi wa kituo cha afya Nyankumbu, ujenzi wa uwanja wa michezo Geita mjini, ukaguzi wa mradi wa maduka ya CCM na uwanja wa maonesho pamoja na kutembelea makundi maalum yanayojishughulisha na shughuli za kiuchumi ambao wamekopeshwa na Halmashauri ya Mji Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa