Kamati Ya Lishe Geita Mji Yapata Ujuzi Bukombe
Wajumbe wa Kamati ya lishe ya Halmashauri ya Mji wa Geita wakiongozwa na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndugu Janeth Mobe pamoja na wanavikundi viwili vya wanawake na vijana wanaonufaika na mkopo wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, unaotolewa na Serikali wamefanya ziara ya mafunzo katika eneo la Runzewe Kata ya Uyovu Wilayani Bukombe.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe Ndg. Janeth Mobe amesema kuwa ziara hiyo imefanyika tarehe 14/9/2022 kwa kuwatembelea kikundi cha Bora kilimo-Biashara ambacho kinajishughulisha na uchakataji wa nafaka na uzalishaji wa unga lishe wenye virutubishi vyenye Asidi ya foliki, Vitamin B12, Madini ya chuma na madini ya zinki.
Bi. Mobe ameongeza kuwa ziara hiyo imefanywa baada ya kutambua umuhimu wa Halmashauri ya Mji Geita kujifunza namna ya kuzalisha unga wa mahindi na muhogo wenye mchanganyiko wa madini na vitamini ambao una faida mbalimbali zikiwemo kuzuia upungufu wa damu, kuongeza ukuaji wa mwili na akili, kuongeza ulaji wa vyakula vyenye viini lishe, kuongeza uwezo wa kujifunza na kuelewa pamoja na kuzuia matatizo ya kiafya yatokanayo na upungufu wa vitamin na madini. Hivyo unga huo ni muhimu kwa wanafunzi wa shule za Geita mji ambazo zina hosteli na mabweni.
Kikundi cha Bora-Kilimo Biashara kilianzishwa mwaka 2014 kikiwa na idadi ya wanachama watano ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu waliojiunga pamoja na kujikita kwenye masuala ya kilimo na ufugaji ambao walipatiwa sehemu ya mtaji wao na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe na kufanikiwa kununua mashine moja ya kusaga na baada ya miaka kadhaa walipanua biashara yao kwa kuongeza mashine ya kukoboa mahindi, kukoboa mchele na kuuchambua kulingana na viwango tofauti.
Mpaka sasa kikundi hicho kimefanikiwa kuwa na ofisi mbili na sasa wanajenga mashine ya kukamua alizeti, kutengeneza ajira ya vijana 19 kutoka kwenye maeneo ya mradi wao ambao wanafanya shughuli mbalimbali za kiwandani hapo. Vijana hao pia wamefanikiwa kupata masoko ya bidhaa zao kutoka kwenye shule za bweni, kusafirisha nchi za jirani kama Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa