Jamii Yatakiwa Kuwalinda Watoto Dhidi ya Ukatili
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe amewakumbusha wazazi/walezi mkoani Geita kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kikamilifu katika malezi ya Watoto na kuwalinda dhidi ya vitendo vya kikatili vinavyoendelea katika jamii.
Mhe. Cornel Magembe ametoa kauli hiyo Tarehe 16 Juni 2023 alipokuwa akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika Shule ya Msingi Uwanja Geita mjini.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amesema kuwa ni wajibu wa wazazi au walezi kuhakikisha Watoto wanasoma vyema, wanapatiwa chakula,huduma za afya na kutokomeza mila kandamizi zinazopelekea kuwepo kwa ndoa za utotoni,ubakaji, ulawiti, ajira za Watoto na ukatili wa aina yoyote.
Akisoma risala kwa niaba ya watoto wa mkoa wa Geita Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Watoto mkoa wa Geita Joseph Mkombozi amesema kuwa Watoto mkoani Geita bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya wazazi kuwatumia Watoto kama kitega uchumi kwa kuwaagiza kuingia mtaani kuomba fedha au kufanya biashara ndogondogo na kukosa nafasi ya kupata malezi ya wazazi baada ya kuonekana katika ulimwengu wa sasa wazazi na walezi wengi wamebanwa na shughuli za kujitafutia kipato Zaidi kuliko kuzungumza na Watoto wao.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Geita Magembe Jackson amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la wimbi la Watoto wa mtaani Pamoja na wazazi/ walezi kutoonyesha ushirikiano kwa wadau wanaosimamia afua za Watoto pindi wanapowafanyia ukatili kutambuliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kupitia maadhimisho hayo Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za mtoto likiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Bi. Paulina Majogoro wametoa vifaa mbalimbali ikiwemo baiskeli za magurudumu kwa Watoto 20 wenye mahitaji maalum, sare za shule sambamba na kufanikisha Watoto 2,000 kupata vyeti vya kuzaliwa.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakumbusha wazazi/ walezi na jamii juu ya malezi, ulinzi wa Watoto na kuwatimizia haki zao za msingi. Maadhimisho yam waka huu yaliongozwa na kauli Mbiu isemayo “Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa kidigitali.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa