Jamii Yatakiwa Kulipa Kipaumbele Suala la Lishe
Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Ndugu Lucy Beda ameiasa jamii katika Halmashauri ya Mji Geita kuhakikisha suala mtambuka la lishe linapewa kipaumbele kwa kuwapatia wajawazito, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na walioko shule wanapatiwa chakula bora chenye vitamini zote na madini mbalimbali.
Katibu Wilaya ya Geita ameyasema hayo hivi karibuni alipomuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita kwenye kikao cha uhamasishaji wa utekelezaji wa mkataba wa lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Nyerere EPZ Bombambili Geita mjini kikiwahusisha Madiwani wote wa Halmashauri ya Mji Geita.
Ndg. Lucy Beda amewaasa Waheshimiwa Madiwani kuwa mabalozi wazuri ambao watatumika kufikisha elimu ya lishe kwa jamii na kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri katika kuhakikisha Halmashauri haibadili matumizi ya vifungu vya bajeti za lishe kwa ajili ya shughuli nyingine zinazoibuka.
‘’Waheshimiwa Madiwani mna wajibu wa kutetea upatikanaji wa elimu endelevu kuhusu desturi nzuri za ulaji, usindikaji na uhifadhi wa chakula na kuhamasisha matumizi ya vyakula vya asili na vinavyopatikana katika maeneo ya walaji, pia mjitahidi kuwahamasisha wanaume wajihusishe na kushiriki katika upangaji wa namna ya kuboresha desturi za ulaji na lishe kwenye familia zao. ‘’ Aliongeza Ndg. Lucy Beda.
Akizungumza juu ya umuhimu wa jamii kuwekeza kikamilifu katika masuala ya lishe, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Geita Bw. Matovu Muhihi amesema kuwa lishe duni hudumaza ukuaji wa Watoto kimwili na kiakili na kuathiri ukuaji wa akili unaopelekea kupungua uwezo wa kufanya vizuri shuleni na pia hupunguza ufanisi katika maisha ya utu uzima, kwa hiyo ni muhimu kuwekeza kwenye lishe ili kuwa na jamii ya watu wenye afya nzuri ya mwili na akili wenye uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya taifa.
Halmashauri ya Mji Geita kama zilivyo halmashauri nyingine hupimwa utekelezaji wake wa afua mbalimbali za lishe kwa kutumia viashiria vilivyo katika mkataba wa lishe unaotekelezwa katika ngazi ya halmashauri na kata kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 ya Chama Cha Mapinduzi( CCM).
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa