Jamii Yatakiwa Kuepuka Uharibifu wa Mazingira
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela ameiasa jamii mkoani Geita kuachana na tabia ya kukata miti hovyo kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama kilimo, ufugaji, uchomaji mkaa na ukataji miti kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ametoa kauli hiyo aliposhiriki katika zoezi la upandaji miti wakati wa maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa yaliyofanyika kimkoa katika Kata ya Lulembela wilayani Mbogwe hivi karibuni.
Mhe. Shigela ameagiza kuwa kila familia inatakiwa iweke utaratibu wa kupanda walau miti mitano kila mwaka ili kupendezesha mazingira na kupata faida nyinginezo zitokanazo na miti.
“Ndugu zangu miti ndio kila kitu katika Maisha yetu, tunapata maji kupitia miti, tunategemea miti kupata mvua za uhakika kwa ajili ya kutuwezesha kulima kwa uhakika na kuvuna mazao mengi, tunapata dawa za mitishamba kwa ajili ya kutibu maradhi mbalimbali kutoka kwenye majani, magome, matunda na mizizi ya miti. Hivyo kila mmoja wetu atambue kuwa uharibifu wa mazingira ndio chanzo cha mabadiliko ya tabia ya nchi na tusipokuwa makini mabadiliko hayo yatagharimu vizazi vyetu vijavyo kwa kiasi kikubwa Zaidi kuliko hali ilivyo kwa sasa.” Aliongeza Mhe. Shigela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhe. Costantine Morandi amewataka wananchi kutimiza wajibu wa kupanda miti kuanzia ngazi ya familia ili kuirejesha hali ya mkoa wa Geita kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na misitu mikubwa sana lakini sasa hivi watu wamekuwa na desturi ya kukata miti hovyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Lee Joshua amesema Serikali inajitahidi kuhamasisha wananchi, taasisi na wadau wote walioko katika mnyororo wa utunzaji mazingira kupanda na kuhifadhi miti lakini mwitikio bado ni mdogo, hivyo viongozi wote wa vijiji, mitaa hadi kata wafanye suala la upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kama agenda yao ya kudumu. Kadhalika doria za mara kwa mara ziendelee ili kudhibiti wananchi wanaoharibu misitu kwa makusudi Pamoja na kuendelea kutoa elimu ya utunzaji wa misitu ili kuwa na uelewa wa Pamoja juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Maadhimisho ya Siku ya upandaji miti kitaifa mwaka 2023 yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania ya kijani bila miti hakuna uhai” ambayo inahamasisha jamii kuacha kuharibu misitu na kuendelea kupanda miti ili kufikia lengo la upandaji miti kimkoa ambapo kila Halmashauri inatakiwa kupanda miti milioni moja na nusu kwa mwaka, kuanzia Oktoba 2022 hadi sasa Halmashauri ya Mji Geita imeshapanda miti 750,000 sawa na asilimia 50% ya lengo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa