Jamii Yashauriwa Kuwapeleka Watoto Kwenye Chanjo
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe ametoa wito kwa wazazi wa jinsia zote kuhakikisha wanawapeleka Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kupata chanjo ambazo zitawakinga na kuwalinda dhidi ya maradhi mbalimbali yanayozuilika kwa chanjo.
Mhe. Magembe ametoa kauli hiyo tarehe 24/4/2023 alipokuwa akizungumza na wazazi waliojitokeza kwa wingi katika viwanja vya Zahanati ya Nyankumbu Geita mjini katika uzinduzi wa Maadhimisho ya wiki ya chanjo kwa mkoa wa Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali afya za wananchi wake kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, ujenzi wa zahanati na vituo vya kutolea huduma za afya zikiwemo hospitali kubwa Pamoja na kuwezesha kampeni mbalimbali zenye lengo la kuboresha afya za watu.
βIli Watoto wetu wanufaike na chanjo, tunao wajibu wa kuwapeleka kwenye kliniki kupitia utaratibu uliopangwa ili wapatiwe chanjo tangu kuzaliwa kwao hadi mtoto anapotimiza umri wa juma 6,10 na 14 pamoja na chanjo ya surua mtoto anapotimiza umri wa mwaka mmoja na nusu. Hivyo ndugu zangu baba na mama tafadhali tutumie fursa hii kuwapeleka Watoto wakachanjwe katika wiki hii ya maadhimisho na baada ya wiki ya chanjo huduma zitaendelea katika vituo vyote vya kutolea huduma ya afya.β Aliongeza Mkuu wa Wilaya ya Geita.
Mratibu wa chanjo Mkoa wa Geita Bi. Wille Luhangija amesema kuwa katika maadhimisho hayo Mkoa wa Geita umelenga kuwafikia Watoto 12,237 wenye umri chini ya miaka mitano waliopo katika ratiba ya chanjo na Watoto 1763 waliopo nyuma ya ratiba ya chanjo na wasichana 9067 wenye umri wa miaka 14 kwa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi ambao wengi wao wapo shuleni.
Bi. Luhangija ameongeza kuwa chanjo zitakazotolewa katika zoezi hilo ni zilezile ambazo hutolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika ratiba ya kawaida ya utoaji huduma za chanjo. Chanjo hizo ni salama na hutolewa bila malipo yoyote na wataalam wenye ujuzi. Hivyo wazazi wanatakiwa kufuata ratiba ya chanjo kwa Watoto na kuepukana na upotoshwaji kuhusiana na huduma zote za chanjo.
Maadhimisho ya wiki ya chanjo 2023 yamebebwa na kauli mbiu isemayo β Tuwafikie wote kwa chanjo, jamii iliyopata chanjo, jamii yenye afya.β
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa