Halmashauri Zaagizwa Kuwekeza Kwenye KKK
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameziagiza Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Geita kuhakikisha wanatenga bajeti katika mipango yao ili kuwezesha mafunzo ya kusoma, kuhesabu na kuandika yanafanyika mara kwa mara kwa walimu wanaofundisha madarasa ya awali kwenye shule za msingi kwa sababu ndiyo msingi wa kumjenga mtoto kitaaluma.
Mhandisi Robert Gabriel ametoa agizo hilo tarehe 18/2/2020 katika Ukumbi wa kituo cha Moyo wa Huruma Geita mjini alipokuwa akifungua rasmi mafunzo ya KKK kwa walimu wa shule za msingi kutoka katika kata za Buhalahala na Kalangalala zilizoko Halmashauri ya Mji wa Geita, mafunzo ambayo yameandaliwa na Shirika la Plan International.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amelishukuru Shirika la Plan kwa kutambua umuhimu wa kuwekeza katika msingi wa elimu kwa mtoto ambayo ni madarasa ya awali na kuandaa mafunzo hayo muhimu, pia kwa kuchangia katika miradi mbalimbali ikiwemo kujenga wadi za wagonjwa katika vituo vya afya, kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum shule ya msingi Mbugani pamoja na masuala mbalimbali ya kijamii yanayoendelea katika Mkoa wa Geita.
“Serikali ya Mkoa wa Geita itahakikisha inayaenzi mazuri yote yanayofanywa na mashirika mbalimbali kama Plan International, kadhalika nawaasa walimu wote mliopata fursa ya kushiriki katika mafunzo haya mtakaporejea katika vituo vyenu vya kazi muhakikishe wanafunzi wenu wa awali wanamudu vyema stadi za kuhesabu, kusoma na kuandika.” Aliongeza Mhandisi Robert Gabriel.
Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Plan International, Meneja wa Plan Mkoa wa Geita Ndg. Adolf Kaindoa amesema kuwa Shirika lake linatekeleza mradi wa Elimu katika Halmashauri za Geita Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwenye shule 12 za msingi ambapo malengo ya mradi huu ni kuboresha uwezo wa walimu wa madarasa ya awali kufundisha mbinu bora zitakazowawezesha watoto kusoma, kuandika na kuhesabu kwa umahiri uliokusudiwa.
Ndg. Kaindoa ameongeza kuwa Shirika la Plan International limeweza kuboresha elimu ya awali kwa njia mbalimbali kama kutoa mafunzo ya KKK kwa wathibiti ubora wa shule, Afisa Taaluma wa shule, maafisa elimu msingi kutoka katika Halmashauri mbili za Wilaya ya Geita, kutoa mafunzo ya KKK kwa walimu wa madarasa ya awali , walimu wakuu na maafisa elimu kata 130,kuhamasisha jumuiya za wazazi na walimu kutoa chakula shuleni ili kuongeza uwezo wa watoto kujifunza na kufaulu pamoja na kutoa vifaa vya shule kwa watoto wenye uhitaji na kutoa taulo za hedhi kwa watoto wa kike walio shuleni.
Meneja wa Shirika la Plan katika Mkoa wa Geita amefafanua kuwa shirika lake limefanikiwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa kutekeleza masuala mbalimbali ambayo baadhi ni kujenga shule ya msingi Mkoani, kujenga madarasa, bweni la wasichana na kisima cha maji chenye sola na bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Ihanamilo, Kujenga shule ya watoto wenye mahitaji maalum na kutoa vifaa vya shule katika Shule ya msingi Mbugani Pia kutoa mafunzo ya ushonaji kwa kutumia vyerehani 50 kwa watoto 100 wa kike wanaoishi katika kaya maskini, kutoa kadi za CHF( mfuko wa Afya wa jamii ulioboreshwa) kwa watoto 6,216 kutoka katika kaya zisizojiweza kiuchumi.
Mafunzo ya KKK yanafanyika katika Wilaya ya Geita ambayo yatafanyika kwa awamu nne katika kata 4 na kushirikisha walimu na Maafisa elimu kata 379 pamoja na viongozi wa Idara ya elimu Mkoa na Wilaya ya Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa