Halmashauri Zaagizwa Kusimamia Matumizi ya Vitabu
Halmashauri sita za Mkoa wa Geita ambazo ni Mbogwe, Nyang’hwale, Bukombe, Chato, Geita Mji na Geita Wilaya zimetakiwa kuhakikisha vitabu vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya wanafunzi vinafikishwa katika shule husika na vinagawanywa kwa walengwa.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. AveMaria Semakafu wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa usambazaji wa vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu darasa la tano. Uzinduzi uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu Geita Mjini tarehe 22/12/2018.
Dkt. AveMaria Semakafu amesema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya walimu wakuu na viongozi katika ngazi za Mikoa na Halmashauri kuvihifadhi vitabu kwenye makabati na stoo badala ya kuwapa wanafunzi vitabu hivyo wajisomee . “ Cheo ni dhamana, wahusika wote katika kamati za usambazaji wa vitabu mhakikishe vitabu vinafika mahali husika na si kufungiwa makao makuu ya Mkoa au Halmashauri”. Aliongeza Dkt. Semakafu
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu alibainisha umuhimu wa vitabu hivyo kuwa ni kuwawezesha wanafunzi kupata muda binafsi wa kujisomea baada ya masomo darasani kwa lengo la kuongeza udadisi na ujuzi zaidi. Pia aliwataka walimu wakuu kutoa taarifa katika ngazi zinazohusika endapo vitabu havitafika shuleni kwa muda muafaka.
Dkt. AveMaria Semakafu alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Geita kwa mkakati wa Mkoa katika kuhakikisha miundombinu inatosheleza wanafunzi kwa kuongez a vyumba vya madarasa. Kadhalika aliwasihi wazazi na wakazi wote wa Mkoa wa Geita kujitolea kujenga vyumba vya madarasa katika shule za Sekondari ili kuondokana na uhaba wa miundombinu katika shule za Sekondari.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba ameeleza kuwa shughuli ya uandishi wa vitabu ilianza mwezi Februari 2018 ambapo jumla ya nakala 166,737 kwa masomo saba na viongozi vya mwalimu 14,273 zitatolewa kwa Mkoa wa Geita. Pia katika awamu ya kwanza mikoa ya Kigoma, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Geita itapata vitabu na kufikia mwezi Januari 2019 zoezi la usambazaji litakuwa limekamilika katika mikoa iliyosalia.
Jumla ya zaidi ya Shilingi Bilioni 6.8 za kitanzania kutoka katika mapato ya ndani ya Serikali zimetumika kuchapa na kusambaza vitabu zaidi ya nakala milioni 3.5 kwa nchi nzima katika uwiano wa kitabu kimoja kutumiwa na wanafunzi watatu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa