Halmashauri Yatakiwa Kuendelea Kutoa Mikopo ya Wanawake
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mheshimiwa Leonard Bugomola ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Mji Geita kuhakikisha asilimia nne ya mapato ya ndani ya Halmashauri inayotakiwa kutolewa kama mkopo kwa vikundi vya wanawake wanaojishughulisha na kazi mbalimbali za uzalishaji mali zinatolewa kwa wakati.
Mhe. Bugomola ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika katika ngazi ya Halmashauri kwenye viwanja vya soko kuu Geita mjini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji aliongeza kuwa Serikali inathamini na kutambua jitihada za wanawake katika kujishughulisha na kazi mbalimbali za maendeleo kama ufugaji mifugo, biashara ndogondogo na nyinginezo ambazo zinawawezesha kujikwamua kiuchumi wao binafsi, familia zao na Taifa kwa ujumla. Hivyo kama fedha hizo hazitatolewa kwa wakati zitakwamisha mipango mikakati ya kina mama hao.
Akisoma taarifa ya wanawake wa Mji wa Geita Bi. Rehema Mteta amesema kuwa wanaishukuru Halmashauri ya Mji Geita kwa kuwapatia mikopo katika vipindi tofauti ambapo mikopo hiyo imewawezesha wanawake kuondokana na mfumo dume unaowafanya kina mama kuwa tegemezi kwa waume zao, pia wamekuwa wakichangia pato la Taifa kwa kulipa kodi katika shughuli zao za kiuchumi na idara ya maendeleo ya jamii wamekuwa mstari wa mbele kutoa mafunzo ya mara kwa mara juu ya elimu ya ujasiriamali na namna ya kuboresha shughuli zao.
Bi. Mteta amebainisha changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni kusubiri mikopo kwa muda mrefu baada ya kuwasilisha fomu za maombi, Baadhi wa wanawake kutorejesha mikopo waliyoichukua kwa wakati ili iweze kutolewa kwa waombaji wengine. Pia kina mama wachache kutokuwa waaminifu na kutokomea na mikopo waliyopatiwa na Halmashauri kwa malengo ya kujiendeleza kiuchumi.
Siku ya wanawake Duniani huadhimishwa tarehe 8 kila mwaka Duniani kote kwa lengo la kutambua jitihada zinazofanywa na wanawake wote katika kujikwamua kiuchumi ambapo kauli mbiu ya mwaka 2019 ni “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa