Halmashauri ya Mji Yakabidhiwa Miti 3000
Jumla ya Miche ya miti 3000 imekabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji Geita kwa lengo la kuhakikisha miti hiyo inapandwa katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Geita ili kutunza mazingira na kutengeneza muonekano mzuri wa mji.
Akipokea miche hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita hivi karibuni Ofisini kwake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Ndugu Thomas Dimme amewashukuru wajasiriamali hao kwa kutambua wajibu wao wa kutunza mazingira. Pia wamechangia utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kila Halmashauri inatakiwa ipande miche ya miti 1500.
“Nawapongeza kwa moyo wenu na nia ya dhati ya kutambua wajibu wenu wa kuhifadhi mazingira na kutekeleza Ilani yaUchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015-2020 inayosisitiza kuendelea kusimamia sera na sheria ya mazingira na ushirikihwaji wa jamii katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yenu. Pia nawasihi muendelee kushirikiana na Serikali katika shughuli nyingine za ujenzi wa miradi ya maendeleo zinazoendelea katika maeneo yenu.” Aliongeza Katibu Tawala wa Wilaya.
Afisa Misitu wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndugu Lee Joshua akipokea miti hiyo kwa niaba ya Halmashauri amewashukuru wananchi hao kwa kufanya jambo jema kwa mara ya kwanza kwa kutambua kuwa mazingira yameharibika na ameomba wadau wengine wenye uwezo kuiga mfano ili waweze kunusuru mazingira yao na kuondokana na tabia nchi.
Ndg. Lee Joshua amesema kuwa miche ya miti hiyo itagawanywa 500 kwa kila shule na kupandwa katika shule za Msingi Mwatulole, Nyantorotoro, Buhalahala na shule za Sekondari Bulela, Bung’wangoko na Ihanamilo zilizoko Halmashauri ya Mji wa Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa