Halmashauri Yahimizwa Kukamilisha Miundombinu Ya Shule Kwa Wakati
Viongozi na wataalamu wote wanaosimamia ujenzi wa miundombinu ya madarasa, mabweni na vyoo vya wanafunzi wamesisitizwa kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inayojengwa katika shule za awali, msingi Pamoja na Sekondari kupitia mradi wa BOOST na wafadhili mbalimbali unakamilika kwa wakati ili ianze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa( TAMISEMI) Bwana Sospeter Mtwale alipofanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Geita na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni matatu ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Geita ambayo yanajengwa kwa Shilingi Milioni 360 kutoka Serikali kuu na vyumba vinne vya madarasa Pamoja na choo cha wanafunzi vinavyojengwa kwa fedha za huduma ya kampuni kwa jamii kutoka Kampuni ya Barrick Tanzania.
Bw. Mtwale ametoa shukrani kwa kampuni ya Barrick kwa fedha za utekelezaji wa miundombinu hiyo na kuipongeza Halmashauri ya Mji Geita kwa usimamizi mzuri na kueleza kuwa lengo la ziara yake mkoani Geita ni kukagua miundombinu ya elimu inayojengwa na Serikali ya awamu ya sita Pamoja na wafadhili mbalimbali. Pia kuhimiza uwajibikaji na usimamizi wa miradi hiyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Upanuzi wa miundombinu ya kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Geita kupitia fedha za Serikali ukamilike kwa wakati kwa kuzingatia ubora wa thamani ya fedha itakayotumika, kadhalika mafundi wanaojenga majengo hayo wanatakiwa kusimamiwa ipasavyo na wahandisi wa halmashauri katika hatua zote za ujenzi ili kupata majengo yenye ubora na yanayoendana na fedha iliyotolewa.” Aliongeza Bw. Mtwale.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Zahara Michuzi amesema amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wataalamu wengine wakiwemo mafundi wanaojenga miundombinu hiyo kusimamia ujenzi kikamilifu na kuhakikisha wanakamilisha ndani ya wakati uliopangwa ili miundombinu hiyo iweze kuwanufaisha wanafunzi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa