Vikundi 28 vyawezeshwa na Halmashauri ya Mji Geita
Vikundi 20 vya wanawake na 8 vya vijana vinavyojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi vimeongezewa nguvu na Halmashauri ya Mji wa Geita baada ya kukabidhiwa hundi zenye jumla ya Shilingi 133,000,000/=( milioni mia moja na thelathini na tatu) ambazo ni uwezeshaji wa wananchi kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na wanawake.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo kwa vikundi hivyo tarehe 2/5/2017 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Halmashauri ya Mji Geita kwa kutekeleza kikamilifu agizo la Serikali la kuhakikisha wanatumia asilimia 10 ya makusanyo yao kuboresha utekelezaji wa shughuli za vikundi vya wanawake na vijana.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewaasa wanavikundi waliopewa mkopo huo kutumia fedha hizo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazofanya na si kwa matumizi mengineyo ambayo hayakuwepo kwenye mpango. Pia waendelee kutumia elimu ya Shirika la kuhudumia viwanda vidogo( SIDO) ili washauriwe kufanya shughuli ambazo zitawakwamua kiuchumi.
“Acheni mawazo ya kudhania fedha za mkopo mnazopewa ni zawadi ambazo mnaweza kutumia mnavyopenda, bali mnatakiwa kuzitumia fedha hizo katika shughuli za uzalishaji na kuzirejesha kwa wakati ili ziweze kukopeshwa kwa vikundi vingine”. Kauli aliyotoa Mbunge wa Geita Mjini, Mheshimiwa Costantine J. Kanyasu wakati wa hafla ya makabidhiano ya mkopo.
Kwa upande wa mwakilishi wa wakopaji, Makamu Mwenyekiti wa kikundi cha Neema kutoka mtaa wa Mbugani katika kata ya Kalangalala Bi. Naomi John ameishukuru Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwapatia mkopo ambao wamefuatilia kwa kipindi kirefu pasipo mafanikio. Amesema kuwa watatumia mkopo huo kuendeleza biashara yao ya duka la vitenge kutoka duka la rejareja kuwa la jumla.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa Halmashauri imekuwa ikiviwezesha vikundi kukuza mitaji yao ili waweze kutekeleza shughuli za kiuchumi kwa ufanisi kwa kupewa mikopo yenye riba nafuu. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mikopo yenye thamani ya Shilingi 175,000,000 imeshatolewa kwa vikundi vya vijana na wanawake.
Mhandisi Modest Apolinary ameongeza kuwa Halmashauri inaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa sugu ambao wameshindwa kurejesha fedha kwa wakati ili kuhakikisha fedha inayotolewa kwa vikundi husika inatumika kwa mujibu wa taratibu na kurejeshwa ziweze kukopwa na vikundi vingine.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa