Halmashauri ya Mji Geita Yajipanga kukusanya Bilioni 5 Mwaka 2018/2019
Halmashauri ya Mji Geita imekisia kukusanya jumla ya Shilingi 5,114,157,735 toka vyanzo vya ndani ambayo fedha hii imejumuishwa katika jumla ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 ambayo ni Shilingi 44,983,794,197.00.
Akiongea wakati wa kikao cha Baraza Maalum la Bajeti lililoketi Tarehe 01/3/2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Geita kwa lengo la kupitisha bajeti ya Mwaka wa fedha 2018/2019, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mheshimiwa Leonard Kiganga Bugomola amesema kwa mwaka wa fedha uliopita Halmashauri ilipanga kukusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 5, ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2017 Halmashauri imeweza kukusanya kiasi cha Shilingi 2,868,353,850.15 sawa na asilimia 52.
Mh. Bugomola ameongeza kuwa kutokana na mafanikio ya ukusanyaji uliofikia nusu ya makadirio ana imani kuwa mpaka kukamilisha mwaka wa fedha 2017/2018 mwezi Juni mwaka huu, Halmashauri itakuwa imefikisha lengo la makusanyo. Aidha makusanyo hayo yanatoa mwanga wa mafanikio katika bajeti iliyopitishwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa Halmashauri inategemea kukusanya mapato yake kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kama kodi ya huduma( service levy) kutoka kampuni ya Mgodi wa Dhahabu Geita na Kampuni nyingine zinazofanya kazi na Mgodi huo, kodi ya nyumba za kulala wageni, Leseni za biashara,faini mbalimbali, upigaji chapa mifugo na ushuru wa mifugo, ushuru wa mazao mbalimbali na matunda.
“Katika Bajeti ya mwaka 2018/2019. Jumla ya Shilingi 15,585,248,344 zimetengwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, Kiasi cha shilingi 24,632,539,165 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi 4,765,976,688 kwa ajili ya matumizi mengineyo”. Aliongeza Mhandisi Modest Apolinary.
Katika Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019, Halmashauri ya Mji Geita imejielekeza katika kufikia vipaumbele vyenye shabaha na malengo ambayo ni Kuendelea kuboresha na kuimarisha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani ili kuongeza mapato ya Halmashauri, Kuboresha Sekta za huduma za jamii, hususan, Elimu, Afya, Maji, Barabara, Mifugo, Uvuvi, Kilimo, Misitu, Maendeleo ya Jamii, Ushirika,
Kusaidia Sera ya Taifa kufikia Uchumi wa kati wa uendelezaji wa viwanda na Kuimarisha Utawala bora.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa