Geita Yaibuka kidedea katika Olimpiki maalum
Wanafunzi watano walioshiriki Mashindano yanayowashirikisha watu wenye ulemavu wa akili yanayofahamika kama Olimpiki maalum( special Olympics) yaliyofanyika Mjini Zanzibar hivi karibuni wameibuka na ushindi ambapo wanafunzi watatu kutoka katika Shule tano zinazofundisha elimu maalum katika Halmashauri ya Mji Geita wamepata medali za dhahabu, shaba na fedha.
Mwanafunzi Mathias Donald kutoka Shule ya Msingi Mbugani amerejea na medali tatu ambapo aliibuka mshindi wa kwanza katika mchezo wa riadha mita 400 na mchezo wa kuruka na kupata medali mbili za dhahabu, na mshindi wa pili riadha mita 800 na kupewa medali ya shaba kati ya washiriki 600 kutoka Tanzania nzima walioshiriki katika mashindano hayo.
Akiongea wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza wanafunzi hao iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Geita, Afisa Elimu Mkoa wa Geita Bi. Rehema Mbwilo ametoa pongezi kwa watoto walioibuka washindi kwa kujituma kikamilifu na kuuletea heshima kubwa Mkoa wa Geita kutokana na ushindi hususani mshindi wa kwanza katika mchezo wa riadha.
Afisa Elimu Mkoa pia amemshukuru Mkurugenzi wa Mji Geita kwa kutambua umuhimu wa watoto wenye ulemavu wa akili kushiriki michezo hiyo kwa kuwagharamia wanafunzi hao waliowakilisha timu ya Mkoa wa Geita.
Bi. Mbwilo ametumia fursa hiyo kuwashauri wazazi wa watoto wenye ulemavu wa akili kuwapeleka shule watoto wao ili kuwapa haki ya elimu. “ Mwitikio wa wazazi kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu katika Mkoa wa Geita bado ni mdogo kwani idadi ya watoto walioko shule ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watoto ambao wamefungiwa majumbani. Watoto hawa wakielimishwa watajitambua na watajifunza fani mbalimbali za ufundi stadi, hivyo msiwanyime fursa hiyo muhimu kwao”. Aliongeza Afisa Elimu Mkoa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Mhandisi Modest Apolinary amewapongeza vijana hao kwa ushindi hodari na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kikamilifu katika kuibua vipaji walivyojaliwa. Pia amewaahidi kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali watajitahidi kukamilisha bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Mbugani na kuwapatia mahitaji muhimu ya kujifunzia ili watambue kuwa wao ni watu wa muhimu katika jamii waliyomo.
Jumla ya wanafunzi watano kutoka katika shule zinazofundisha elimu maalum katika Halmashauri ya Mji Geita waliuwakilisha Mkoa wa Geita katika mashindano ya Olimpiki maalum mjini Zanzibar hivi karibuni yakiwa na lengo la kuwapa fursa watu wote wenye ulemavu wa akili kujiona ni raia wenye manufaa, pia kuwa wazalishaji wanaokubalika na kuheshimika katika jamii zao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa