Geita Mji Yavuka Lengo Ukusanyaji Mapato
Halmashauri ya Mji Geita imefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2022/2023 uliokamilika mwezi Juni 2023.
Akisoma taarifa ya makusanyo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani katika ukumbi wa EPZA Bombambili, Mkuu wa Kitengo cha fedha na uhasibu Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Kasaija Katikiro amesema kuwa Halmashauri kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato imefanikiwa kufikisha lengo hilo kutokana na uwazi na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ambayo imeongeza imani na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.
Ndg. Katikiro ameongeza kuwa Halmashauri ya Mji imezingatia masuala muhimu kama kuimarisha usimamizi wa mapato ya ndani kwa kufanya tathimini na kuibua vyanzo vipya vya mapato, kutumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato na kupanga matumizi katika maeneo ya vipaumbele.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na biashara wa Halmashauri ya Mji Geita ameongeza kuwa uelewa wa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi, upatikanaji wa takwimu sahihi juu ya idadi ya walipa kodi, sehemu kubwa ya mapato ya ndani kufanya kazi ya ujenzi na uendelezaji wa miradi mbalimbali katika jamii kumeongeza uaminifu baina ya Serikali na wananchi pamoja na ushirikiano baina ya watumishi wa idara ya fedha na idara nyingine ni masuala yaliyochangia kufanikisha ukusanyaji wa mapato uliovuka malengo.
Kwa upande mwingine Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Geita limetoa pongezi za dhati kwa idara za elimu msingi na Sekondari kwa kufanya kazi kwa bidii na kusimamia miradi yao kikamilifu wakati wa utekelezaji hali ambayo imepelekea kuwa na miradi yenye viwango vya hali ya juu ambayo imewawezesha wanafunzi waishio katika kata mbalimbali kupata fursa ya elimu.
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Geita Bw. Rashid Muhaya amepokea pongezi hizo na kusema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi milioni 60 zimetengwa kwa ajili ya kumalizia nyumba za walimu Pamoja na vyumba vya maabara katika Shule za sekondari zilizopo nje ya mji ili kuwezesha wanafunzi wao kupata elimu bora pasipo vikwazo vyovyote.
Katika mwaka wa fedha uliokamilika mwezi Juni 2023 Halmashauri ya Mji Geita ilipanga kukusanya Shilingi Milioni 12.18 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Milioni 12.36 sawa na asilimia 101.53%.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa