Geita Mji Yasaini Utekelezaji Miradi ya TACTIC
Halmashauri ya Mji Geita imesaini mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) ambapo ujenzi wa Barabara za kilomita 17 kwa kiwango cha lami zitajengwa kupitia mradi huo.
Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika tarehe 23/09/2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa .
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Costantine Morandi ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia Halmashauri yake fedha nyingi ambazo zitawezesha mji wa Geita kuwa na ongezeko la barabara za lami ambazo zitapunguza kero ya ubovu wa barabara iliyokuwepo kwa kipindi kirefu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Zahara Michuzi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuikumbuka Halmashauri ya Mji Geita kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania ambapo ameahidi kushirikiana na watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi za mitaa kuhakikisha Barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha hali ya juu na zinakamilika kwa wakati ili ziweze kuwanufaisha wananchi.
Barabara zinazojengwa kupitia mradi wa TACTIC katika Halmashauri ya Mji Geita ni Barabara ya Nyamalembo- Kivukoni Sekondari- Nyankumbu senta Km 3.9, Barabara ya Mkolani- Mwatulole senta Km 5.9, Barabara ya Samandito- Emma Mama Kengele- Mwabasabi senta Km 4.8 na Barabara ya Mshinde Twiga Road Km 2.4, ujenzi wa barabara hizi utatekelezwa na Mkandarasi SICHUAN ROAD AND BRIDGE( GROUP) CORPORATION wa jijini Dar es Salaam.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa