Geita Mji Yapongezwa Kwa Utekelezaji Mzuri wa Miradi
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Mji Geita kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Magembe ametoa pongezi hizo tarehe 30 Oktoba 2023 alipokuwa katika ziara ya kukagua miundo mbinu ya elimu na afya inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Mji Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia Halmashauri ya Mji wa Geita fedha nyingi za ujenzi wa shule mpya, madarasa, ukarabati wa shule kongwe na ukarabati wa hospitali chakavu.
“Napenda kutumia fursa hii kukupongeza Mwalimu Ally Dauda, Mkuu wa Shule ya Sekondari Geita kwa kusimamia miradi vizuri na kwa uaminifu mkubwa, shule yako imepatiwa zaidi ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, madarasa na vyoo vya wanafunzi ambapo ubora wa miradi hiyo unaonekana Dhahiri na umekuwa mwepesi sana wa kufanya marekebisho ambayo yamebainishwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali”. Aliongeza Mhe. Magembe.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amewataka wahandisi wa Halmashauri ya Mji Geita kufuatilia na kukagua maendeleo ya miradi mara kwa mara ili kujiridhisha na ubora wa miradi inayojengwa na pia kuhakikisha miradi inakamilishwa kwa wakati ndani ya muda uliopangwa ili iweze kutoa huduma kwa walengwa waliokusudiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Geita Mwl. Ally Dauda ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa mabweni, madarasa na choo kwani baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaboresha mazigira na kuwaongezea wanafunzi ari ya kusoma kwa bidi kwa sababu mabweni waliyokuwa wakitumia awali ni chakavu.
Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi Mhe. Magembe ametembelea ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Nyantorotoro ambayo imefikia asilimia 80 ya ujenzi kupitia fedha za Serikali kuu, Ujenzi wa mabweni 3 ya wanafunzi, madarasa 4, choo cha matundu 6, ujenzi wa jengo jipya la upasuaji na jango jipya la kutunzia maiti katika Hospitali ya Mji Geita pamoja na ukarabati wa majengo yaliyochakaa katika Hospitali hiyo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa