Geita Mji Yapongezwa Kuvuka Lengo la Upandaji Miti
Halmashauri ya Mji Geita imepongezwa kwa kufanikiwa kupanda miti 1,500,451 kwa mwaka 2022/2023 ambayo ni sawa na asilimia 100.03% ya lengo la Taifa.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 25/09/2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Selemani Saidi Jafo alipokuwa akizungumza na wananchi kabla hajazindua zoezi la upandaji miti katika eneo la EPZA Bombambili ambapo Maonesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanaendelea.
Mhe. Jafo amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa agizo kwa kila Halmashauri kuhakikisha inapanda miti milioni moja na laki tano kwa kila mwaka ambapo Halmashauri ya Mji Geita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za Umma na binafsi, Shule za Msingi na Sekondari, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wamefanikiwa kupanda miti kwa zaidi ya asilimia 100.
Waziri Jafo amewaagiza wananchi kuendelea kupanda miti kuanzia mitano kwenye makazi yao na sehemu za kazi na kuitunza vyema ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na miti iliyopandwa na jamaa zao. Pili kwa kuendelea kupanda miti watatunza mazingira na kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Mabadiliko ya Tabianchi.
“Nawaagiza Wakala wa Misitu Tanzania watoe vitalu vya miti vya kutosha ili wananchi wasikose miti ya kupanda na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) watengeneze mkaa mbadala wa kutosha na wabainishe maeneo utakapokuwa unapatikana ili wananchi waupate wakati wote na si kusubiri kipindi cha Maonesho pekee.” Aliongeza Mhe. Jafo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Ndugu Lee Joshua amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na uhamasishaji uliofanywa na kitengo ambapo wataalam wa misitu hutembelea mashamba ya wakulima kwenye Shule za Msingi na Sekondari ambapo wanafunzi wana wajibu wa kuhakikisha wanatunza miti waliyopanda. Pia Taasisi mbalimbali na watu binafsi wameendelea kuhamasishwa juu ya umuhimu wa kupanda miti katika maeneo yao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa