Geita Mji Yapitisha Bajeti ya Tsh. Bilioni 60.2 Mwaka 2024/2025
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Geita limepitisha Bajeti ya Shilingi 60,214,506,780.00 ambayo inategemea kukusanywa na kutumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe ameagiza kuwa miradi iliyopangwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025 itekelezwe kikamilifu kwa kiwango kinachoridhisha ili Imani ya wananchi kwa serikali ya awamu ya sita iendelee kuwa kubwa. Pia wataalam wote wahakikishe wanapeana ushirikiano katika ukusanyaji wa mapato katika vyanzo mbalimbali vilivyobainishwa.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti kwa niaba ya Mkurugenzi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani lililoketi hivi karibuni katika ukumbi wa EPZA Bombambili Geita mjini kwa lengo la kupitisha bajeti hiyo, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Samson Ndaro ameeleza kuwa kati ya fedha hizo shilingi 19,464,148,060.00 ni fedha za Mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo bajeti mpya ina ongezeko la asilimia 16.8% zaidi ya ile ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Ndg. Samson Ndaro amefafanua kuwa maeneo ya kipaumbele katika bajeti yam waka wa fedha 2024/2025 ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali, ukamilishaji wa miradi yote viporo katika sekta za elimu, afya na utawala ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma stahiki pamoja na kuendelea kuhimili athari zitokanazo na kudorora kwa Uchumi wa dunia na kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma katika soko la dunia.
Afisa Mipango amebainisha maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu na kupata viongozi wanaotokana na ridhaa ya wananchi, uendelezaji wa ardhi katika maeneo ya mijini na vijijini kwa kufanya upimaji wa viwanja vya Taasisi za Umma, kuimarisha mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii hasa katika sekta za afya, elimu, utawala na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano ya Barabara.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa