Geita Mji Yapitisha Bajeti 2019/2020
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Geita limepitisha makadirio ya Shilingi 49,312,038,078 katika kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo Mishahara, matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti hiyo wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani tarehe 21/01/2019 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji, Afisa Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Sylvia Rwehabura amesema kuwa Halmashauri ya Mji imeandaa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2019/2020 kwa kuzingatia maelekezo ya Mwongozo wa kitaifa wa miaka mitatu, mipango shirikishi ya jamii na vipaumbele vya Halmashauri.
Bi. Rwehabura ameongeza kuwa Halmashauri ya Mji imezingatia masuala muhimu kama kuimarisha usimamizi wa mapato ya ndani kwa kufanya tathimini na kuibua vyanzo vipya vya mapato, kutumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato na kupanga matumizi katika maeneo ya vipaumbele.
Kwa upande wa sekta mbalimbali Halmashauri ya Mji imejipanga kutenga maeneo ya viwanda, kilimo na mifugo, nyuki,vituo vya kutolea huduma za jamii, kiuchumi na utawala za miundombinu ya afya, maji, elimu, misitu ya jamii, maeneo ya maafa na stendi. Pia kuhakikisha kamati za watu wenye ulemavu, mabaraza ya wazee na kamati za kutokomeza ukatili dhidi ya mtoto na mwanamke zinaanzishwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika sekta ya utawala Halmashauri imefanikiwa kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa soko la Kalangalala ambalo lina majengo mawili, jengo moja likiwa ni kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na lina vizimba 108 na jengo la pili ni ghorofa lenye sakafu ya chini na juu kwa ajili ya biashara za kibenki na duka kubwa (supermarket).
Katika mwaka wa fedha 2019/2020 mapato yanayotegemewa kukusanywa na kupokelewa ni mishahara shilingi 33,690,176,760.31, matumizi ya kawaida ni shilingi 886,895,000, miradi ya maendeleo shilingi 8,084,872,892 na mapato ya ndani ya Halmashauri ni shilingi 6,425,993,950 ambazo zinafanya jumla ya shilingi 49,312,038,078 zinazokadiriwa kutumiwa na Halmashauri ya Mji wa Geita katika kutekeleza majukumu mbalimbali .
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa