Geita Mji Yang’ara Ukusanyaji wa Mapato
Halmashauri ya Mji wa Geita imeibuka kidedea kati ya Halmashauri za Miji 22 Tanzania Bara katika ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Halmashauri ya Mji wa Geita imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi 5,931,976,537.38/= sawa na asilimia 107.57% ambapo malengo ya makusanyo yalikuwa ni Shilingi 5,514,320,052.00/=
Akizungumza wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii Mwekahazina wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Munguabela Kakulima amesema kuwa sababu zilizopelekea mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ni pamoja na uwazi na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ambayo imeongeza Imani na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.
Mwekahazina wa Halmashauri ya Mji wa Geita ameongeza kuwa uelewa wa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi, upatikanaji wa takwimu sahihi juu ya idadi ya walipa kodi, sehemu kubwa ya mapato ya ndani kufanya kazi ya ujenzi na uendelezaji wa miradi mbalimbali katika jamii kumeongeza uaminifu baina ya Serikali na wananchi pamoja na ushirikiano baina ya watumishi wa idara ya fedha na idara nyingine ni masuala yaliyochangia kufanikisha ukusanyaji wa mapato uliovuka malengo.
Kwa upande wake Afisa Mapato wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Goodluck Nkwabi amefafanua kuwa ufuatiliaji wa karibu wa makusanyo katika vyanzo mbalimbali vya mapato na ushuru wa vibanda ambayo ni tozo mpya iliongezeka kutoka shilingi elfu 10 hadi shilingi 30,000/= kuanzia mwezi Januari 2018 sababu iliyowezesha kupandisha kwa kasi makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Akibainisha mikakati iliyowekwa katika mwaka mpya wa fedha 2018/2019 Ndg. Kakulima amesema kuwa Halmashauri imejipanga kuimarisha kanzu data( Data base) ya walipa kodi ili kuweza kutambua walipa kodi wa zamani na wapya, sambamba na kuanzisha madaftari ya walipa kodi katika kila mtaa na kata shughuli inayofanywa kwa ushirikiano na watendaji wa mitaa.
Ndg. Kakulima ameongeza kuwa ujenzi ulioanza hivi karibuni wa maduka ya kisasa kuzunguka soko kuu la Geita mjini ambayo yanajengwa kupitia fedha za Miradi ya jamii( CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wachenjuaji na wachomaji wa dhahabu baada ya Serikali kudhibiti uvushaji wa kaboni kutoka Mkoa wa Geita kwenda mikoa ya jirani kutaongeza mapato ya Halmashauri kwa mwaka mpya wa fedha ulioanza mwezi Julai 2018.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa