Geita Mji Yajipanga Utatuzi wa Kero za Wananchi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Yefred Myenzi ameeleza kuwa Halmashauri yake imeanzisha utaratibu wa watendaji wa vijiji, mitaa na kata kuorodhesha kwenye rejista maalum kero na malalamiko yote yanayowasilishwa katika ofisi zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Myenzi alipokuwa akitoa taarifa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kujadili taarifa za robo ya pili 2023/2024 kilichoketi tarehe 15/02/2023 katika ukumbi wa Nyerere EPZA Bombambili.
Ndg. Myenzi amefafanua kuwa Geita Mji imefikia kuanzisha utaratibu huo baada ya kubaini kuwa baadhi ya kero zinazowasilishwa na wananchi katika ofisi za Serikali kwenye maeneo yao lakini zisipopatiwa ufumbuzi kunakosekana kumbukumbu za malalamiko hayo pindi zinapofuatiliwa na viongozi kwa lengo la kuzitatua.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe ametoa agizo kwa watendaji wa vijiji, mitaa na kata kutatua malalamiko yote yaliyo ndani ya uwezo wao yanayowasilishwa katika ofisi zao na kwa changamoto ambazo zitawashinda waziwasilishe katika ofisi ya Mkurugenzi ili kupunguza idadi kubwa ya wananchi wanaopeleka malalamiko yao kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Mhe. Magembe ametoa pongezi za dhati kwa Waheshimiwa madiwani, Mkurugenzi pamoja na wataalam wa Halmashauri ya Mji Geita kwa ukusanyaji mzuri wa mapato katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Disemba 2023, pamoja na usimamizi hodari wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Prudence Temba amepokea pongezi kutoka kwa viongozi na kuahidi kuwa pongezi hizo zitawahamasisha kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuwaasa Madiwani wenzake kwa kuwataka kila mmoja kutimiza majukumu yake katika maeneo yao kwa lengo la kuwapatia wananchi maendeleo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa