Geita Mji Yafanikiwa Kupunguza Msongamano Wa Wanafunzi
Sera ya Serikali ya wamu ya Tano ya Elimu bila malipo imeendelea kuongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa shule kila mwaka. Katika kuendana na kasi ya Halmashauri ya Mji wa Geita imefanikiwa kujenga Shule mpya 10 za msingi na 6 za Sekondari ambazo zimepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la msongamano wa wanafunzi darasani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary ameeleza kuwa Halmashauri imekuwa ya kwanza kwa Halmashauri za miji chini kwa ukusanyaji wa mapato ghafi, jambo ambalo limewawezesha kujenga shule za msingi na Sekondari ili kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafuzi hao.
Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Mji Geita imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa kwa shule za msingi ili kuendelea kupata madarasa ya kutosha na wanafunzi kupata fursa ya kujifunza kwa nafasi.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Ndg. Rashid Mhaya amesema kuwa Halmashauri shule kumi zilizojengwa zimeifanya Halmashauri ya Mji kuwa na shule 16 za sekondari zinazohudumia wanafunzi 14,175 ambapo kabla ya ujenzi wa shule mpya wanafunzi walilazimika kutembea kati ya kilomita 8 hadi 10 kwenda shule jambo ambalo lilikuwa hatari hasa kwa wasichana lakini kwa sasa wanatembea chini ya kilomita tatu kufika shule.
Mwalimu Leo Elias, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyanguku amebainisha kuwa shule hiyo ambayo ni mpya imejengwa kwa ushirikiano baina ya Halmashauri na wazazi ili kurahisisha wanafunzi kufika shuleni kwa wakati kwa sababu walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda kata jirani kusoma Shule ya Sekondari Ihanamilo.
“Licha ya madhara ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wanafunzi wa Kata ya Nyanguku walipokuwa wanakwenda kusoma shule iliyoko katika kata jirani walikuwa wanachoka sana na kushindwa kujifunza vizuri darasani lakini sasa hali hiyo haipo pia wanafunzi wa kike wameweza kuepuka vishawishi vya barabarani walipokuwa wakitembea umbali mrefu.” Ameongeza Mwalimu Leo.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyanguku Rajab Faida amesema kabla ya kujengewa shule iliyoko jirani na nyumbani walipata shida kufika shule ya Sekondari Ihanamilo kwani wanafunzi ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwanunulia baiskeli walitembea kwa miguu umbali mrefu ambapo baadhi waliishia vichakani kwa sababu ya kuchelewa kufika shule na kuogopa kuadhibiwa.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Geita Bw. Maclaud Mero ameeleza kuwa katika shule mpya kumi zilizojengwa wamejenga vyumba 117 vya madarasa na matundu ya vyoo 82 vitakavyowezesha wanafunzi kupata elimu bora na yenye kiwango. Bw. Mero anaeleza kuwa msongamano wa wanafunzi una athari kubwa katika mchakato wa kujifunza kwani mwanafunzi hawezi kupata maarifa yaliyokusudiwa kwa sababu mwalimu anakwama kuwafikia wanafunzi wote, vipindi vinapotea, walimu kushindwa kusahisha kazi za wanafunzi kwa wakati mambo ambayo hatma yake ni kushusha kiwango cha ufaulu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Manga, Lugasia Nyatega amefafanua kuwa shule hiyo imezalishwa kutoka Shule ya Msingi Nyakabale ambayo ilikuwa na wanafunzi wengi baadhi yao wakitembea umbali mrefu kufika shule. Pia ametoa ushuhuda wa wanafunzi 10 ambao waliacha masomo katika Shule ya Msingi Nyakabale kutokana na umbali mrefu lakini baada ya kujengwa shule mpya ya Manga wanafunzi hao wameripoti shule na wanaendelea na masomo.
Pamoja na Shule mpya zilizojengwa Halmashauri ya Mji imefanikiwa kujenga nyumba sita za walimu katika Shule ya Sekondari Bung’wangoko ambazo zimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 150 kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania.
Shule mpya za Msingi zilizojengwa ni pamoja na Kabuyombo, Nyantindiri, Bombambili, Magogo B, Manga, Kaseni, Machinjioni, Kakonda, Tumaini na 14 Kambarage. Shule za Sekondari ni Nyakabale, Mgusu, Nyanguku, Nyanza, Nyabubele na Lukaranga.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa