Geita Mji Yabuni Mkakati Wa Uboreshaji Usafi
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi taka na Usafi wa Mazingira Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Aloys Mutayuga ameeleza kuwa Halmashauri yake imeanza kutekeleza mradi wa maboresho ya ukusanyaji, uhifadhi na uchakataji wa taka kwa lengo la kuimarisha usafi wa mazingira na kuongeza mapato kupitia taka.
Kupitia mradi huu wananchi watapata furs aya kutupa aina mbalimbali za uchafu katika chombo maalum kwa aina ya taka aliyonayo, mfano chupa za maji, mabaki ya vyakula, makaratasi nk hayatachanganywa katika chombo kimoja bali kila aina ya taka itatupwa katika chombo chake kilichobainishwa kwa maandishi yanayosomeka katika masanduku hayo.
Ndg. Mutayuga amebainisha hayo hivi karibuni wakati wa zoezi la kusambaza makontena Matano ya kuhifadhia taka kwa kila kituo katika vituo kumi mjini Geita ili kutoa fursa kwa watupa taka kutenganisha taka na kurahisisha uchakataji.
“Utenganishaji wa taka utafanikisha mradi wa Halmashauri wa kuzifanyia taka urejeshaji(recycling) kwa kuzalisha mbolea kutoka taka ozo, kuzalisha mkaa kwa makaratasi na taka za plastiki ambazo zitauzwa viwandani. Pia zoezi hili litatuwezesha kutambua aina ya takataka inayozalishwa kwa wingi katika mji wa Geita kuliko takataka nyinginezo.” Aliongeza Aloys Mutayuga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Zahara Michuzi amesema kuwa taasisi yake imejipanga kutenga bajeti ya kutosha ili kuhakikisha mradi wa uchakataji taka unafanikiwa na kuwa endelevu kwa lengo la kuimarisha usafi wa mji na kuongeza mapato kila mwaka wa fedha.
Bahati Godwin ambaye ni mkazi wa Geita mjini ametoa pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwawekea vifaa vingi vya kutupia taka katika maeneo mbalimbali ya makazi yao na kuahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kila mwananchi ameelewa matumizi sahihi ya vifaa hivyo.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na Kitengo cha Usimamizi taka na Usafi wa Mazingira hadi sasa Halmashauri ina uwezo wa kukusanya tani 2800 kati ya tani 5700 za taka zinazozalishwa kwa mwezi, saw ana ufanisi wa asilimia 49 huku lengo likiwa ni kufikia ufanisi wa asilimia 60 katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa