Geita Mji Kuanza Utekelezaji wa Mradi wa TACTIC
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 22 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa kilomita 17 za Barabara kwa kiwango lami ya zege (Asphalt Concrete) katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji Geita kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania(TACTIC).
Akizungumza wakati wa mkutano wa kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa EPZA Bombambili Geita mjini tarehe 24/10/2023, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia Geita Mji fedha nyingi za utekelezaji wa mradi huo utakaoleta maendeleo kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Geita ameeleza kuwa kwa niaba ya wananchi wa Mji wa Geita wameupokea mradi huo kwa moyo mkunjufu na kuwaelekeza watendaji na wenyeviti wa mitaa kuhakikisha wanafikisha taarifa sahihi za kuanza kwa mradi huu kwa wananchi katika mitaa yote inayopitiwa na Barabara hizo ili wananchi watoe ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
“Mkandarasi uliyepewa dhamana ya ujenzi wa Barabara katika mji wetu nawaagiza kuhakikisha anajenga Barabara hizo katika ubora wa hali ya juu na kukamilika ndani ya miezi 15 kama walivyokubaliana kwenye mkataba ili mradi huo uweze kuwanufaisha wananchi na Wilaya nzima kwa ujumla”. Aliongeza Mhe. Cornel Magembe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Bw. Lee Joshua amesema kuwa baada ya mradi kukamilika utabadilisha muonekano wa mji wa Geita, kutoa ajira kwa wananchi wa Mji wa Geita kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na utekelezaji wa mradi huo pamoja na kupunguza msongamano wa magari na vyombo vingine vya usafiri.
Mwakilishi wa Mkandarasi M/s Sichuan Road & Bridge (Group) Corporation Limited wa Dar es Salaam ambaye amesaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo utakaoanza mapema mwezi Novemba 2023 Ndg. SIBO ameahidi kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalam wa Halmashauri na Wakala wa Barabara vijijini na mjini(TARURA), Viongozi kuanzia ngazi ya mtaa, kufuata mkataba unavyoeleza. Kuajiri wafanyakazi kulingana na sheria za Nchi na kukamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa na katika kiwango cha hali ya juu.
Mradi wa Ujenzi wa Kilomita 17 za Barabara Geita mjini utakuwa chini ya Mkandarasi Mshauri M/s Luptan Consults Limited akishirikiana na SAFI Consultants Limited wa Dar es Salaam ambapo Barabara zitakazojengwa ni Barabara ya Mkolani- Mwatulole km 5.9, Nyankumbu- Kivukoni km 3.9, Ngunzombili-Samandito-Emma-Mama Kengele km 3.3, Mwatulole-Mshinde- Twiga- Geita Gold Refinery km 3.9
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa