Geita Mji Kinara Utoaji Mikopo kwa Vikundi
Halmashauri ya Mji wa Geita imekuwa Halmashauri ya kwanza katika Mkoa wa Geita kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, mikopo isiyo na riba ambayo ni asilimia 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wakati wa hafla fupi ya utoaji Hundi kwa vikundi 40 iliyofanyika katika Ukumbi wa Gedeco Halmashauri ya Mji Geita Tarehe 12/7/2019 Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Majagi Maiga amesema kuwa Halmashauri ya Mji Geita imefanikiwa kutoa jumla ya Shilingi 706,000,000/=( Milioni Mia saba na sita) kwa vikundi 149 katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Ndg. Majagi amefafanua kuwa kiasi cha Shilingi 419,000,000/= zimekopeshwa kwa vikundi 93 vya wanawake, Shilingi 262,000,000/= zimekopeshwa kwa vikundi 51 vya vijana na vikundi 5 vya watu wenye ulemavu vimekopeshwa Shilingi 25,000,000/=. Pia vikundi vinaendelea kurejesha ambapo hadi mwaka wa fedha unaisha jumla ya Shilingi 52,235,000/= zimerejeshwa kutoka kwa baadhi ya vikundi vilivyokopeshwa.
Akiongea wakati wa kukabidhi hundi kwa vikundi 40 vya awamu ya mwisho kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amewaasa wanavikundi waliopatiwa mkopo kutambua kuwa fedha wanazokopeshwa ni maalum kwa ajili ya kuwasaidia kutekeleza mipango waliyopanga kwa ajili ya kujipatia maendeleo na si fedha ya kufanyia starehe au shughuli binafsi zisizo na manufaa.
Mhandisi Robert Gabriel ametumia fursa hiyo kuwaagiza wataalam wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutembelea vikundi na kufanya tathmini ili kubaini vikundi hai vyenye malengo na vinafanya vizuri kwenye shughuli zao. Kadhalika vikundi vipatiwe uwezo ili vipate ushauri wa namna ya kuendesha biashara zao ili kuwawezesha wanakikundi kutimiza malengo yao.
Bi. Anneth Jummanne mwanakikundi wa Yes we can social group kutoka mtaa wa Kagera kata ya Kalangalala ametoa shukrani kwa kuwatambua na kuwapa mikopo isiyo na riba. Pia wameahidi kuzitendea haki fedha walizopewa kwa kuzitumia katika shughuli zao za ujasiriamali na kuzirejesha kwa wakati.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa