Geita Kunufaika Na TASAF Awamu ya Nne
Kiasi cha Dola milioni 50 zimetengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa mpango wa kupunguza umaskini na uendelezaji wa miundombinu ya kutolea huduma za jamii kama elimu, afya na maji katika mikoa mitano ambayo ni Geita, Mwanza, Simiyu, Arusha na Njombe kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Akizungumza wakati wa kikao kazi cha kujenga uelewa wa Pamoja juu ya mradi wa kupunguza umaskini awamu ya nne na kubadilishana uzoefu kutoka kwa waratibu wa Mkoa wa Geita katika ukumbi wa Uwekezaji kiuchumi Bombambili Geita mjini hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladslaus Mwamanga ameshauri kuwa kusiwe na mrundikano wa utoaji wa huduma katika eneo moja bali fursa zitawanywe kwenye maeneo yenye uhitaji yatakayobainishwa na wanajamii wa maeneo husika.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Staki Senyamule ameishukuru Serikali chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zenye lengo la kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa pia kulinda maslahi ya familia zao na jamii kwa ujumla.
Mhe. Senyamule ameongeza kuwa matarajio ya viongozi ni kuwa utekelezaji wa miradi hii utatoa njia mbadala za ajira kwa walengwa na kuwawezesha kushiriki katika kazi za jamii ili kupata kipato cha ziada kwa matumizi ya kaya ambacho kitawawezesha kuboresha miundombinu ya kijamii, kuwajengea ujuzi na stadi za Maisha walengwa watakaoshiriki katika kazi na kugharamia mahitaji mbalimbali ya msingi kwenye kaya zao.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewaagiza wasimamizi wote wa kisekta kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji wa mradi na kuepuka ubadhirifu au uhujumu wa fedha na vifaa, tabia hiyo haitavumilika bali hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya msimamizi au kiongozi yeyote atakayebainika.
“Kukamilika kwa miradi itakayopangwa kwa viwango vilivyowekwa na kutoa huduma kwa walengwa kwa wakati kitakuwa ni kipimo tosha cha ufanisi wenu katika kutekeleza majukumu ya kila siku kwa ajili ya maendeleo endelevu wanayotamani kuyafikia wananchi wa Mkoa wa Geita. Hivyo wataalamu mnatakiwa kutekeleza miradi yote kwa weledi na kuzingatia miongozo.” Aliongeza Mhe. Senyamule.
Diwani wa Kata ya Kalangalala Mhe. Prudence Temba ambaye alimuwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuukumbuka Mkoa wa Geita katika mradi huo na kuwashauri viongozi wa TASAF kuwapatia elimu hiyo Madiwani wote ili wasaidie katika usimamizi wa miradi ambayo itatekelezwa katika maeneo yao ya utawala kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa