Geita Gold FC Yazindua Mfumo Wa Usajili Wanachama
Timu ya mpira wa miguu Geita Gold Footbal Club inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Geita imezindua mpango wa kusajili wanachama wa klabu hiyo kwa lengo la kuwafanya wanachama kuwa sehemu ya umiliki wa klabu.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari hivi karibuni, Katibu Mtendaji wa Klabu hiyo Ndg. Simon Shija amesema kuwa mpango huo unatekelezwa kwa mujibu wa katiba ya klabu na utatoa fursa kwa watanzania wenye mapenzi na timu ya Geita Gold ndani nan je ya mkoa wa Geita kupata kadi za uanachama.
“Kwa mujibu wa katiba ya klabu Ibara ya 5 inawatambua wanachama kama sehemu ya kuiongoza klabu na kufanya maamuzi. Licha ya kuwa klabu hii inamilikiwa na Halmashauri kwa sehemu kubwa imeona vyema kutoa nafasi kwa mwanachama kuwa sehemu ya umiliki ambapo tumekusudia kupokea wanachama wasiopungua elfu mbili kwa mwaka kama sehemu ya kuimarisha timu.” Aliongeza Simon Shija.
Katibu wa Timu ya GGFC ameeleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 10 ya katiba ya timu inazungumzia ada za wanachama, ambapo kwa mwezi kila mwanachama ataichangia kadi kwa Shilingi 3000. Matarajio ya awali ni kusajili wanachama 2,000 ndani ya mkoa wa Geita na kupata angalau shilingi milioni 72 kwa mwaka itakayoongeza mapato ya klabu ambayo ni wastani wa Shilingi Bilioni 1.6. Aidha baada ya mwanachama kusajiliwa atapokea kadi yake ya uanachama iliyo katika mtindo wa kidijitali.
Mpango wa kusajili wanachama ni endelevu na timu inafanya jitihada kubwa kuimarisha mfumo huo na kuwa na klabu yenye ukubwa na ushindani lakini pia kuongeza nguvu ya kiuchumi ndani ya klabu. Ndugu Simon Shija amesema kuwa wanazingatia uwepo wa wanachama kutoka pande zote za Tanzania na wamezindua namba maalum ya kuchangia na kulipia ada ya uanachama kupitia LIPA NAMBA 5215290 Geita Gold . Pia klabu imeingia mkataba na kampuni ya N-card kwa ajili ya kutengeneza kadi za wanachama na timu inarajiwa kucheza michezo ya kirafiki vijijini kuhamasisha wananchi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa