Geita Gold FC Yakabidhiwa Basi la Wachezaji
Timu ya Mpira wa miguu ya Geita Gold FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji Geita imekabidhiwa basi litakalotumika kusafirishia wachezaji katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya michuano ya Ligi kuu ya NBC na mashindano mengine.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya basi hilo lililogharimu Shilingi Milioni 500 kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya GGML Terry Strong amesema kwa miaka mingi kampuni yake imekuwa ikiona Fahari kuisaidia jamii inayowazunguka kupitia utekelezaji wa miradi na shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo udhamini mkuu kwa Timu ya mpira wa miguu ya Geita Gold.
Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla fupi ya makabidhiano ya basi hilo iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Soko kuu la Dhahabu Geita mjini amesema kuwa upatikanaji w abasi hilo kunatokana na matunda ya mabadiliko ya sheria ya madini, kanuni na sera inayoitaka Kampuni kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii(CSR)
Mhe. Mavunde ametoa pongezi za dhati kwa kampuni ya GGM kwa udhamini walioufanya ambao ni mkubwa sana katika kuitangaza timu, kampuni yao pamoja na raslimali ya dhahabu inayopatikana kwa wingi katika mkoa wa Geita, na kuwaalika wadau wengine wa maendeleo katika mkoa wa Geita kuiga mfano wa GGM katika kuidhamini timu yao katika masuala mbalimbali yanayohitajika.
Mbunge wa Geita mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu ameushukuru uongozi wa GGM kwa udhamini huo kwani kabla ya kuwepo kwa basi hilo kulisababisha wachezaji kusafiri kwa magari madogo ya coaster na viongozi wao kupanda mabasi kwa nauli zao.
Mhe. Kanyasu amewasihi wachezaji wa Geita Gold kutambua namna wananchi wa Geita wanavyoipenda na kuiamini timu yao hivyo wanapokuwa uwanjani watambue maumivu wanayoyapata wananchi hao baada ya wachezaji kucheza katika kiwango dhaifu au kufanya mambo ambayo ni kinyume na matarajio ya mashabiki wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Costantine Morandi ametoa shukrani za dhati kwa GGM kwa udhamini huo na kueleza kuwa ukitaka kujua thamani ya mdhamini ni muda wa kutafuta wadhamini, akitolea mfano changamoto waliyoipitia kwa msimu uliopita ambapo walipeleka maombi kwa kampuni zaidi ya ishirini bila mafanikio.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa