Geita Bila UKIMWI Inawezekana
Wadau wa maendeleo katika mji wa Geita wamebaini baadhi ya changamoto ambazo zikitatuliwa zitasaidia kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika mji wa Geita. Changamoto hizo zimebainishwa wakati wa kongamano la kujadili hali halisi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na kuweka mikakati ya kupunguza maambukizi hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji hivi karibuni.
Askofu Stephano Sabuda ambaye ni Mwenyekiti msaidizi wa jumuia ya Interfaith amesema kuwa elimu dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI inatakiwa ifikishwe katika jamii kwa sehemu kubwa. Amefafanua kuwa wananchi waishio maeneo ya vijijini hawana elimu ya kutosha juu ya ugonjwa wa UKIMWI na athari zake katika jamii, hivyo watumishi wa Mungu, watu waishio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI pamoja na wataalamu wa masuala ya UKIMWI kutoka Serikalini na Taasisi binafsi washirikishwe katika utoaji wa elimu hiyo.
Mwenyekiti wa watu waishio na Virusi vya UKIMWI Geita mjini amesema kuwa sehemu kubwa ya watu wanaoishi na maambukizi ya ugonjwa huo bado wamejificha, hawataki kujitangaza hadharani au kuwashirikisha ndugu zao wa karibu. Amesema kuwa kitendo cha kujificha ni kujinyanyapaa wenyewe binafsi na kuendelea kueneza maambukizi katika jamii wanamoishi. Hivyo ametoa wito kwa watu hao kutoficha hali zao za kiafya.
Kwa upande wa mwakilishi wa wazazi amesema kuwa wazazi wanatakiwa wabadilike katika malezi kwani kwa sasa wamesahau wajibu wao kama walezi wa watoto kwa kujishughulisha zaidi na majukumu ya kiuchumi, pia kuvaa mavazi yasiyokuwa na maadili kama wazazi na kuwanunulia watoto mavazi yasiyoendana na maadili ya kitanzania.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mh. Leonard K. Bugomola amewaahidi wanachama wa KONGA kuwa Halmashauri itawalipia kodi ya pango la ofisi na kuagiza idara ya Maendeleo ya Jamii iwapatie mkopo umoja wa watu waishio na Virusi vya UKIMWI ili waweze kujikwamua kiuchumi. Pia amewaagiza walimu wakuu wa shule zote katika Halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha sherehe zote mashuleni zinafanyika mchana na kumalizika saa 12 jioni.
Mratibu wa UKIMWI wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Mariam John amesema kuwa kitengo chake kinaendelea na zoezi la uundaji wa vikundi vya watu waishio na Virusi vya UKIMWI na kuendesha mafunzo ya ujasiriamali ili kujiingizia kipato na kujikwamua kiuchumi, pia kuwakopesha mikopo yenye riba nafuu ili waweze kuanzisha biashara na miradi mbalimbali.
Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka maambukizi mapya 54,000 hadi 56,000 hujitokeza katika nchi ya Tanzania. Kauli mbiu ya maadhimisho ya UKIMWI kwa mwaka 2017 ni “Changia mfuko wa udhibiti wa UKIMWI nchini uokoe maisha, Tanzania Bila UKIMWI inawezekana.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa