Fugeni Nyuki Kibiashara- Kanyasu
Wanavikundi wanaojishughulisha na ufugaji nyuki katika Wilaya ya Geita wameshauriwa kufanya shughuli hiyo kwa malengo ili kufanya ufugaji wa nyuki kuwa wa kibiashara zaidi.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Costantine Kanyasu alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Geita ambao wameunda vikundi vya ufugaji nyuki hivi karibuni katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo pia aligawa mizinga ya nyuki kwa vikundi hivyo.
Mheshimiwa Kanyasu ameongeza kuwa Wizara yake imeamua kufanya zao la nyuki kuwa moja ya zao la kibiashara katika mikoa minane ikiwemo Geita hivyo wakazi wa Geita wanatakiwa watumie fursa hiyo kwa kutofuga nyuki kwa mazoea kama zamani.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii amesema kuwa Serikali itatoa mashine za kisasa kwa ajili ya kuchakata asali katika mikoa yote ya ukanda wa asali hivyo wafugaji hao wanatakiwa wasimamie na kutunza vizuri maeneo ambapo mizinga itawekwa kwa kulinda vyanzo vya maji kwani hakuna maisha ya nyuki bila maji. Pia aliwataka wafugaji kulinda misitu isichomwe moto.
Mheshimiwa C. Kanyasu alitumia fursa hiyo kuwaagiza wataalam wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania kuhakikisha wanakuwa karibu na vikundi vilivyopata mafunzo ya ufugaji nyuki ili kuwasaidia katika shughuli zao za ufugaji na kutatua changamoto zinazowakabili.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya ufugaji Meneja misitu wa Wilaya ya Geita Ndg. Fredy Ndandika amesema kuwa uvamizi na uharibifu wa misitu kwa shughuli za kilimo, ukataji miti, moto kichaa na malisho ya mifugo pamoja na ukosefu wa soko la kudumu la mazao ya nyuki ambayo ni asali na nta ni kati ya changamoto ambazo huathiri maendeleo ya ufugaji nyuki.
Katika ziara yake ya kikazi Wilayani Geita Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Costantine Kanyasu amegawa mizinga ipatayo 200 kwa vikundi 10 kutoka Halmashauri mbili za Wilaya ya Geita ambavyo vilipata fursa ya kuwezeshwa mafunzo ya namna ya ufugaji wa kisasa wa nyuki, mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa huduma za Misitu Wilaya ya Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa