Fanyeni Kazi Kwa Maadili na Ubunifu- RC Geita
Wafanyakazi wa sekta binafsi, mashirika, Taasisi na watumishi wote wa umma katika mkoa wa Geita wameaswa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi katika shughuli zao sambamba na kuongeza ubunifu katika majukumu yao ya kila siku.
Ujumbe huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi duniani tarehe 01/5/2023 yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya CCM Kalangalala Geita mjini.
Mhe. Shigela ameongeza kuwa kila mfanyakazi katika eneo lake la kazi anao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza ufanisi wa kazi na endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kikamilifu basi ataboresha kiwango cha kipato kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewasisitiza waajiri kutenga bajeti ya kuwapeleka watumishi wao kwenye mafunzo mbalimbali kwa lengo la kuboresha maslahi na mazingira rafiki kwa mfanyakazi ili kuongeza tija na ufanisi kwenye taasisi na kukabiliana na changamoto mpya za maendeleo katika utendaji kazi.
Mhe. Shigela amekemea tabia ya baadhi ya waajiri ambao wanahamisha watumishi bila mpangilio wala kuwa na bajeti hiyo, amesema kuwa kuna watumishi wakifanya makosa wanapewa uhamisho kwenda vituo vingine vya kazi kama sehemu ya adhabu,suala hili sio sahihi na lisitishwe mapema iwezekanavyo kwani kumuhamisha mtumishi pasipokuwa na bajeti ni kuiongezea Serikali mzigo. Mtumishi akikosea hatua za kinidhamu zichukuliwe katika eneo lake analofanyia kazi na sio kumuhamisha.
Akitoa salamu za Mei mosi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Zahara Michuzi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wafanyakazi kupitia fedha za miradi mbalimbali kama madarasa na nyumba za watumishi na kuahidi kuendelea kutenga bajeti ya kuwapeleka watumishi wao kila mwaka wa fedha kwenye mafunzo ya muda mfupi na mrefu ili kuendelea kuwa na watumishi mahiri katika fani mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA) Ndg. Obed Mwakapango ameiomba Serikali kuingilia kati katika kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali ambazo bado zinawakabili wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi ikiwemo malimbikizo ya mishahara, taasisi binafsi kutozingatia viwango vipya vya mishahara, na baadhi ya waajiri kutopeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani mwaka 2023 yameadhimishwa kitaifa katika mkoa wa Morogoro na kuhudhuriwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yakiwa yamebeba kauli mbiu isemayo ‘’Mishahara Bora na Ajira za staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni sasa’’.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa