Familia Zahimizwa Kutatua Migogoro Kwa Upendo
Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Margareth Macha ametoa wito kwa familia kuhakikisha wanatatua migogoro yao kwa amani na upendo ili kuepukana na tatizo la kusambaratika kwa familia kunakochangia ongezeko la vitendo vya ukatili katika jamii hususani kwa Watoto.
Bi. Macha ameyasema hayo hivi karibuni alipomuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita wakati wa kongamano la kuhitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambalo limefanyika katika ukumbi wa eneo maalum la uwekezaji kiuchumi Bombambili mjini Geita.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji ameongeza kuwa vitendo vya ukatili ambavyo vimeendelea kushamiri katika jamii kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na vurugu za kifamilia, ambapo baada ya wazazi kugombana na kuachana Watoto wengi wanabaki wanajilea wenyewe hali inayopelekea baadhi ya watu wasio na utu kuwafanyia matendo ya kikatili.
“Asilimia kubwa ya wazazi katika jamii za wachimbaji madini wameacha majukumu ya malezi kwa Watoto baada ya wao Kwenda kutafuta riziki katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji dhahabu. Wazazi mnatakiwa kubadilika na kutimiza wajibu wenu wa malezi ya Watoto na kila mwananchi awe balozi wa mwingine katika kutoa ushirikiano kwa kutoa Ushahidi juu ya matukio ya ukatili wa kijinsia yanapofanyika katika jamii”.
Kwa Upande wake Afisa Maendeleo Mkoa wa Geita Ndg. Elikana Haruni amewaasa wananchi wilayani Geita kuachana kabisa na mila pamoja na desturi ambazo kwa namna moja au nyingine zinaendelea kukandamiza Watoto wa kike na kusababisha ukatili wa kijinsia.
Mtaalam kutoka taasisi ya Marafiki wa Elimu Geita Bw. Ayoub Bwanamadi amewataka wananchi kuripoti matukio yote ya kikatili yanayotokea katika jamii yao na kutomaliza kesi za ukatili kienyeji au kindugu hususan kwa wanawake ambao wanaogopa kuripoti juu ya ukatili unaofanywa na waume zao majumbani kwa hofu ya kuachwa na kuchukiwa na familia za upande wa mume.
Ndugu Bwanamadi ameeleza kuwa jamii inapaswa kutambua kuwa sheria zipo kwa ajili ya utekelezaji wa haki, endapo wananchi wataendelea kuficha matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea kwenye jamii yao kwa kuhofia sheria kuchukua mkondo wake basi matukio hayo hayatatokomezwa asiliani.
Maadhimisho ya kuhitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Kila uhai una thamani,Tokomeza mauaji na Ukatili dhidi ya wanawake na Watoto”. Ambapo yalienda sambamba na hitimisho la wiki ya msaada wa kisheria katika Halmashauri ya Mji Geita iliyobeba kauli mbiu isemayo “Ukatili na Udhalilishaji wa kijinsia ni kikwazo kwa maendeleo ya Taifa, wananchi wote Tusimame kuzuia”.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa