Elimu ya Usafi wa Mazingira yahitajika kwa Wananchi- DC Maganga
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Josephat Maganga amewaagiza wataalam wa Idara ya Mazingira katika Halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha wanatoa elimu ya kina juu ya usafi na utunzaji wa mazingira kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mjini Geita.
Agizo hili limetolewa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyankumbu katika Halmashauri ya Mji wa Geita aliposhiriki zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Mtaa wa Uwanja hivi karibuni, ambapo alikuwa Mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mhe. Josephat Maganga amefafanua kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa usafi na Afya kwa ujumla kuanzia watoto waliofiki kisha umri wa kwenda shule. “Wazazi mnatakiwa kuanza kuwafundisha watoto wenu kutunza usafi wangali wadogo ili jamii iweze kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu . Pia wananchi hamasikeni kupanda miti ya vivuli na matunda.” Aliongeza Mkuu wa Wilaya ya Geita.
Afisa Usafishaji na Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Pancrace Shwekelela amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuacha tabia ya kutupa taka hovyo kama maganda ya ndizi, miwa, mahindi nk badala yake wayatupe katika vifaa maalum vya kutupia taka( dustbin).
Pia Ndg. Shwekelela ameongeza kuwa Halmashauri imejipanga kuunda vikosi kazi vya mitaa ambavyo vitasimamia usafi katika mitaa yao. Vikosi kazi hivi vitasaidia kuhifadhi mazingira kwa kuwaripoti waharibifu wa mazingira ambao watalazimika kulipa faini ya papo kwa papo watakapokamatwa kwa makosa ya kutupa taka hovyo na watoa taarifa hizo watapatiwa zawadi kidogo kwa kazi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Nyankumbu Diwani wa Kata hiyo Mhe. Paschal Kimisha amesema kuwa ukosefu wa barabara katika mtaa wa Uwanja kunafanya miundombinu iliyopo kutokuwa rafiki kwa utunzaji wa mazingira hivyo ametoa rai kwa Wakala wa Barabara Vijijini na mijini( TARURA) kuhakikisha barabara hizo zinachongwa na sheria zilizopo juu ya utunzaji wa mazingira zizingatiwe.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa