Mfumo wa MWEMKWA Mkombozi kwa Watoto
Mfumo wa elimu ya msingi usio rasmi( MWEMKWA) unaowawezesha wanafunzi kuanzia umri wa miaka 9 hadi 13 ambao hawakupata nafasi ya kuanza elimu ya Msingi wakiwa na umri wa miaka 7 kwa sababu mbalimbali umebainika kuwanufaisha watoto wanaoandikishwa katika darasa hilo.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya juma la Elimu katika Halmashauri ya Mji wa Geita Mwalimu Bahati Gabriel kutoka shule ya Msingi Mseto, ambaye ni mwalimu wa darasa la MWEMKWA amesema kuwa wanafunzi wake wanafundishwa kusoma,kuhesabu na kuandika na wakishaelewa wanaingizwa darasa la nne katika mfumo rasmi kwa ajili ya kufanya mtihani wa Taifa, wakishafaulu wanaendelea na darasa la tano pamoja na wanafunzi wengine.
Katika maadhimisho ya juma la Elimu kwa mwaka huu, wataalam wa Idara ya elimu walitembelea shule mbalimbali za msingi ili kukagua shughuli za ufundishaji wanafunzi zinazofanyika kila siku na changamoto wanazokabiliana nazo walimu na wanafunzi katika utendaji kazi wao.
Mwanafunzi wa darasa la MWEMKWA, Marko John amesema kuwa alichelewa kuanza shule baada ya wazazi wake kutengana na kuachwa kijijini na bibi yake ambaye hakuwa na uwezo wa kumnunulia mahitaji ya muhimu kwa ajili ya kuanza shule. Baada ya miaka kadhaa mjomba wake alimchukua na kumleta Geita mjini ambapo alimwandikisha shule. Marko ana malengo ya kuwa Daktari ili aisaidie jamii ambayo haina uwezo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mseto Bi. Grace Mutabuzi amefafanua kuwa watoto wengi wanajilea wenyewe na wengi wao wanafika kujiandikisha shule wao binafsi, ambapo walimu huchukua jukumu la kuwatembelea wazazi/ walezi wa wanafunzi majumbani na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa elimu. Ameeleza kuwa sababu kubwa ya watoto kuchelewa kuanza shule ni kitendo cha watoto hao kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama kilimo, upondaji mawe, uchimbaji mdogo na biashara ndogondogo.
Bi. Grace Mutabuzi amefafanua kuwa changamoto wanazokabiliana nazo katika ufundishaji wa darasa la MWEMKWA ni utoro wa rejereja ambapo baadhi ya wanafunzi hawafiki shule kwa wiki mbili hadi tatu kwa sababu ya kwenda kujitafutia riziki na mahitaji mbalimbali. Pia hakuna ushirikiano baina ya wazazi/walezi na walimu.
Kadhalika Mwalimu Mkuu huyo ameongeza changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wanafunzi huacha shule baada ya kujua kusoma na kuandika. Pia wengine kutofanya mtihani baada ya kusajiliwa, akitolea mfano wa wanafunzi wanne kati ya sita waliokuwa wameandikishwa kwa ajili ya mtihani wa Taifa wa darasa la nne Mwaka 2017 kuacha shule kabla hawajafanya mtihani huo.
Mwalimu Grace Mutabuzi na Afisa Elimu ya Msingi katika Halmashauri ya Mji wa Geita Bw. Yesse Kanyuma wana matumaini ya kuwavusha wanafunzi wa darasa la MWEMKWA ambao wataonyesha bidii ya kufikia ndoto zao, kwani kuna wanafunzi ambao kwa sasa ni walimu, wako vyuo vikuu, wanajishughulisha na biashara zao ambao ni matunda yaliyopatikana kupitia elimu ya MWEMKWA.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa