Elimu ya Lishe Ibadilishe Mazoea katika Jamii- DAS Geita
Kina mama walioko katika Halmashauri ya Mji Geita wameshauriwa kutumia fursa ya elimu ya lishe wanayopatiwa na wataalam wa Kitengo cha lishe ili kubadilisha mazoea ya uandaaji wa uji wa Watoto ambao hauzingatii lishe bora.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Ndugu. Lucy Beda alipokuwa akiongea na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kampeni ya utoaji matone kwa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambayo imefanyika tarehe 05/06/2024 katika kituo cha afya Nyankumbu.
Katibu Tawala Wilaya ya Geita ameeleza kuwa wataalam wa Kitengo cha lishe katika majukumu yao ya kila siku wameendelea kutoa elimu ya uandaaji wa uji wa Watoto kwa kuzingatia makundi sita ya vyakula ambayo ni nafaka mizizi na ndizi za kupika ,mbogamboga,matunda, vyakula vya asili ya nyama, kunde na mafuta na elimu ya unyonyeshaji kwa Watoto wachanga
Hivyo wazazi na walezi waliokuwa na mazoea ya kuweka kundi la wanga pekee kwenye uji wa Watoto wabadilike na kufuata kanuni za uandaaji wa lishe inayofaa kwa makuzi bora ya Watoto na kuepukana na tatizo la udumavu na utapiamlo mkali kwa Watoto.
Kaimu Afisa Tarafa wa Geita mjini Ndugu Cosmas Bayaga ametoa rai kwa wataalam wa kitengo cha lishe kutembelea shule mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu kuhusu maandalizi ya uji wenye mchanganyiko wa makundi yote ya chakula na kuachana na tabia ya kupika uji kwa mazoea.
Kwa upande wa Mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji Geita Daktari Sunday Mwakyusa amesema kuwa changamoto kama uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa kuzingatia makundi sita ya vyakula, matone ya Vitamin A na dawa za minyoo pamoja na mapokeo hasi ya baadhi ya wazazi/walezi juu ya dawa za chanjo hupelekea kutokea kwa magonjwa ya Watoto kama vile minyoo, surau na uoni hafifu.
Dkt. Mwakyusa amesema kuwa Halmashauri ya Mji Geita imejipanga kufikia Watoto 55,710 wenye umri wa miezi 6 hadi 59 ambao watafikiwa kwa njia za kliniki za mkoba, kliniki ya baba, mama na mtoto vituoni na kwenye vituo na kwenye vituo vyote vya kutolea huduma huduma za afya sambamba na kufanya upimaji wa hali ya lishe kwa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa