DC Geita Akoshwa na Mradi wa Madarasa Kasamwa
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Hashim Komba amefurahishwa na ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ndogo ya walimu kwa ajili ya Watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya msingi Kasamwa.
Mhe. Komba ameridhishwa na ujenzi wa madarasa hayo hivi karibuni alipokuwa katika ziara yake ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata ya Kasamwa pamoja na kupokea kero na changamoto za wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Soko la Kasamwa.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameeleza kuwa ujenzi wa madarasa hayo umemkosha kwa sababu umefikia hatua kubwa kwa gharama ya shilingi milioni 30 pekee, jambo ambalo ni la kuigwa mfano kwa sababu maeneo mengine wasingefikisha mradi hatua hiyo kwa fedha hiyo pekee.
Sambamba na ujenzi wa madarasa hayo Mkuu wa Wilaya ya Geita ametoa rai kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita na wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha umaliziaji wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum uendane na uhalisia wa mahitaji ya Watoto hao na pia ujenzi wa mabweni na madarasa ukamilishwe kwa wakati ili viweze kutoa huduma kwa walengwa.
DC Komba ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kuhakikisha kuwa kila mmoja katika nafasi yake anashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanyika katika maeneo yao. Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya jemedari Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajitahidi kufikisha maendeleo kwa wananchi wote kwa kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi hivyo wananchi hawana budi kuunga mkono jitihada hizo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa