Bonanza la Walimu lafana Geita Mjini
Walimu wa shule za msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Geita wamefurahi kushiriki katika mashindano ya michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa wavu, mchezo wa kuvuta Kamba, kukimbiza kuku na kukimbia ndani ya magunia. Michezo iliyofanyika hivi karibuni katika uwanja wa Sekondari ya Kalangalala, Halmashauri ya Mji wa Geita
Wakizungumza wakati wa michezo hiyo Mwalimu Shani Chiza ameshukuru Idara ya Elimu katika Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kutambua umuhimu wa kutenga siku hiyo ambayo imewawezesha walimu kuendeleza vipaji vyao na kupunguza msongo wa mawazo baada ya shughuli za ufundishaji wanazozifanya katika maeneo yao ya kazi.
Mwalimu David Shushu ameongeza kuwa michezo iliyofanyika baina yao na wakuu wa Idara inaboresha undugu na urafiki, inatia hamasa kwa vijana ambao ni wanafunzi kuona jinsi walimu wao wanavyothamini michezo na kuwakutanisha wanamichezo tofauti katika fani mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa Elimu msingi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Yesse Kanyuma amesema kuwa bonanza hilo litakuwa endelevu kwa kila mwaka kwa lengo la kutenga siku maalum kwa ajili ya walimu ni kujenga ukaribu kati ya wakuu wa idara na walimu ili wanapofika kuhudumiwa katika Ofisi za Halmashauri wajisikie vizuri na wajione kama sehemu ya Halmashauri ya Mji wa Geita.
Katika siku hiyo maalum kwa walimu , baada ya michezo kufanyika walimu waliburudika pamoja katika hafla ya jioni iliyopewa jina la “usiku wa mwalimu” ambapo mgeni rasmi katika sherehe hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg. Herman Kapufi ambaye alitumia fursa ya sherehe hiyo kuwapongeza walimu kwa shughuli wanazofanya na kuwaasa kuwa waadilifu katika wito wao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa