Bilioni 9.8 Kutekeleza Miradi Geita Mji Kupitia CSR
Halmashauri ya Mji Geita na Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) wamesaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambayo itatekelezwa kupitia fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kwa kipindi cha miaka miwili 2022 na 2023, ambapo Halmashauri ya Mji wa Geita itatumia Shilingi Bilioni 9.8 katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji Saini wa Mkataba wa makubaliano hayo baina ya Halmashauri ya Mji Geita na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) iliyofanyika tarehe 21/3/2023 katika ukumbi wa Mchauru Village Geita mjini, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Mgodi wa GGM kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwahimiza wawekezaji wengine ndani ya mkoa wa Geita kuiga mfano wa kampuni ya GGM katika kuhudumia jamii inayowazunguka.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewaagiza watekelezaji wa miradi hiyo kuhakikisha mchakato wa kutafuta wakandarasi wa ujenzi wa miradi hiyo uanze mapema ili ifikapo mwezi wa tano mwaka 2023 ujenzi wa miradi hiyo uwe umeanza. Pia fedha zilizoidhinishwa katika hati ya makubaliano zitumike katika miradi iliyoainishwa kwenye mpango wa makubaliano kwa wakati uliopangwa na katika ubora wa hali ya juu ili iweze kuleta tija kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mheshimiwa Costantine Morandi amesema 1/3 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri yake yanatoka kwenye Mgodi wa GGM na yameiwezesha kujenga zahanati Zaidi ya 20 pamoja na utekelezaji wa miradi mingine ya michezo,barabara, elimu na pia vijana kutoka kwenye mitaa inayozunguka mgodi wananufaika na ajira kila mwaka katika mgodi huo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Anglo Gold Ashanti Bw. Simon Shayo amesema kuwa Mgodi wa GGM unatambua thamani ya jamii inayowazunguka hivyo wanajitahidi kuhakikisha wananchi wanaishi vizuri kupitia manufaa ya miradi ya elimu, afya, maji, kilimo, miundombinu ya barabara Pamoja na miradi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Baadhi ya Miradi itakayotekelezwa katika mkataba wa Makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya CSR kwa miaka miwili 2022 na 2023 ni Pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa uwanja wa michezo Geita mjini, ujenzi wa maduka kuzunguka Soko kuu la Dhahabu kwa awamu ya tatu, ujenzi wa daraja litakalounganisha mtaa wa Nyakabale na Kijiji cha Bugulula, Ujenzi wa Uzio katika kituo cha Afya Kasamwa na ukamilishaji wa Zahanati zilizojengwa kwa fedha za CSR miaka iliyopita ili zianze kutoa huduma kwa wananchi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa