Wananchi Wakumbushwa Kulipa Kodi kwa Muda
Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimwa Angelina Mabula amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa Geita kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka ili kutoingia kwenye orodha ya wadaiwa sugu wa madeni ya Serikali.
Mhe. Mabula ametoa kauli hiyo alipokuwa akigawa hati miliki kwa baadhi ya wananchi wakati wa kikao chake na wataalam wa idara ya Ardhi kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Geita, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Nyerere , eneo maalum la uwekezaji kiuchumi Bombambili hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Ardhi amewataka Maafisa Ardhi wateule kusimamia sheria ya ardhi kwa wadaiwa sugu ambao wanaendelea kukaidi takwa la kisheria la kulipa pango la ardhi wanazozimiliki kila mwaka kwa kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe funzo kwa wengine ambao hawatambui umuhimu wa kulipa kodi hiyo.
Mhe. Mabula ametumia wasaa huo kuwakumbusha wataalam wa idara ya ardhi kutoka maofisini na kwenda kuwaeleimisha wananchi katika maeneo yao elimu mbalimbali kama thamani ya ardhi, umuhimu wa kumiliki ardhi na masuala mengine pasipo kusubiri mpaka waletewe malalamiko ya migogoro ya ardhi. Kadhalika amezitaka Halmashauri kusaidia makampuni yaliyofanya shughuli ya upimaji kupata fedha zao baada ya kukamilisha kazi kwani taarifa inaonyesha makampuni yanazidai fedha nyingi Halmashauri.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Fadhili Juma amemshukuru Naibu Waziri wa Ardhi kwa kutembelea mkoa wa Geita na kuwakumbusha Maafisa Ardhi katika mkoa huo kutimiza wajibu wao kikamilifu na amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwa atasimamia utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa na kuhakikisha yanafanyiwa kazi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa