Tumieni Mbolea Za Viwandani Kurutubisha Ardhi- Mhe. Mgumba
Wakulima katika wilaya ya Geita wameshauriwa kuacha kasumba ya kuogopa kutumia mbolea zinazotengenezwa viwandani kuwa zinaharibu ardhi badala yake waendelee kutumia mbolea za asili sambamba na mbolea za kupandia na kukuzia ambazo zinasaidia kurutubisha ardhi na kuwa na kilimo chenye tija.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika Mheshimiwa Omary Mgumba alipotembelea maduka ya kuuza pembejeo za kilimo, kutembelea mashamba ya wakulima na kukagua kiwanda cha kuchambulia pamba Katongo na kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Nyakato katika Kata ya Nyanguku wakati wa ziara yake ya kikazi Halmashauri ya Mji Geita tarehe 11/01/2020.
Naibu Waziri wa kilimo na Ushirika amewataka maafisa ugani kuwa karibu na wakulima katika maeneo yao ya kazi ili kutoa elimu ya mashamba darasa, masuala yahusuyo kilimo na umuhimu wa matumizi ya mbolea ya viwandani katika mazao yao ili kupata mazao bora na mengi kuliko wanavyopata sasa. Pia amewaagiza wazalishaji wote wa mbolea kuwa na maghala nchi nzima katika kila mkoa, kadhalika wauzaji kwenye mikoa huskie waweke mawakala maeneo ya vijijini.
Mhe. Mgumba alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wakulima kulima zao la muhogo kwa sababu limepata soko kubwa kimataifa na kuwataka kuwa na tabia ya kulipa madeni yao ili kutojinyima nafasi ya kupata fursa mbalimbali zinazopangwa na Serikali juu ya wakulima.
Kwa upande wa wauzaji wa pembejeo za kilimo na mifugo katika kata ya Nyankumbu, Machomba Agrovet wamefanikiwa kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa kata tano za Halmashauri ya Mji Geita kwa kushirikiana na kampuni ya YARA na SEEDCO kupitia mashamba darasa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa