Mkurugenzi Abainisha Faida za Ujenzi wa Uwanja Wa Michezo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara M.Michuzi amesema kuwa uwanja wa michezo wa kisasa unaojengwa katika Kata ya Bombambili mjini Geita utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Geita.
Akizungumza hivi karibuni alipotembelea eneo la ujenzi wa uwanja huo kwa ajili ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa fursa hizo zitatokana na kuja kwa wageni wengi watakaofika kutazama michuano ya ligi kuu itakayokuwa inachezewa katika uwanja huo na kueleza fursa kama huduma za hoteli kwa watakaohitaji malazi, huduma za vyakula na usafiri wa aina mbalimbali.
Mkurugenzi Michuzi ameongeza kuwa yeye Pamoja na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Geita wameongeza nguvu za usimamizi wa ujenzi wa uwanja huo kwa kufika eneo la mradi mara kwa mara ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na kuwapa burudani wakazi wa Geita sambamba na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mji wa Geita watakaoweza kuanzisha biashara za aina mbalimbali.
Mhandisi msimamizi wa ujenzi wa uwanja huo Meja Samuel Hagu amesema ujenzi huo unaendelea vizuri na kwa sasa umefikia kiwango cha 21% na unatekelezwa na Mkandarasi mzawa EFQ Company ambaye ameungana na mwenzake Mugoo Construcion kutoka jijini Mwanza chini ya usanifu na ubunifu wa mradi uliofanywa na wataalam wa Halmashauri kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika na Shirikisho la Mpira la Taifa ( TFF).
Baada ya ujenzi kukamilika uwanja huo utakuwa na uwezo wa kubeba watu 12,000 kwa wakati mmoja na unajengwa kwa fedha ya wajibu wa kampuni kwa jamii ( CSR) ya mwaka 2019,2020 na 2021 inayotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita .
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa