Madiwani ni Kitovu Cha Halmashauri – DC Geita
MKuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Fadhili Juma amewakumbusha Madiwani wa Halmashauri ya Mji waGeita kutambua kuwa wao ndio kitovu cha maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Baraza la kwanza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Geita kilichofanyika Tarehe 7/7/2020 katika ukumbi wa GEDECO ambapo Madiwani waliapishwa na kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na Makamu wake.
Mhe. Fadhili Juma amefafanua kuwa endapo wananchi watakosa huduma za msingi katika maeneo yao lawama zote zitaenda kwao kwa sababu wao ndio wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata( WDC) hivyo waende wakawatumikie wananchi katika maeneo yao maana ushindi walioupata ni mkopo kutoka kwao ambao wanatakiwa wakaulipe kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Costantine Morandi amewashukuru Madiwani wenzake kwa kumchagua kuiongoza Halmashauri kwa kipindi cha miaka mitano na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kujenga imani kwa wananchi.
Mhe. Morandi pia alitumia fursa hiyo kuishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kutosubiri vitendo vya rushwa vitendeke katika Halmashauri yake badala yake izuie kabla havijatendeka ili kusaidia wananchi waweze kunufaika na fedha za miradi ya maendeleo.
Mbunge wa jimbo la Geita Mjini Mheshimiwa Costantine J. Kanyasu aliwashukuru wananchi wa Geita kwa kuwaamini na kuwaahidi kuwa yeye binafsi , Madiwani pamoja na wataalamu wote kutoka Idara mbalimbali za Halmashauri watafanya kazi kwa bidii na mshikamano wakilenga kutimiza ahadi walizozitoa kwa wananchi wa Geita mjini wakati wa kampeni.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Geita lina jumla ya Madiwani 19 ambao waliapishwa na kumchagua Mwenyekiti kwa kura zote za ndio na kumchagua Makamu Mwenyekiti Mhe. Joseph Lusana Lugaila Diwani wa kata ya Ihanamilo kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kura 19 zote za ndio.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa